




KITUO cha Usuluhishi (CRC) kinachofanya kazi chini ya Chama cha Wanahabari Wanawakecha (TAMWA) kimejipanga kutoa elimu kwa jamii kuhakikisha kinapambana na matumizi ya pombe kupindukia kwa jamii suala ambalo limezidisha vitendo vya ukatili wa jinsia unaofanywa na watumiaji pombe kupindukia.
Akizungumza na wahariri wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka alisema utafiti uliofanywa na Shirika la IOGT International unaonesha kuwa kiwango cha unywaji pombe jijini Dar es Salaam ni asilimia 47.6 kwa wanaume na asilimia 29 kwa wanawake huku ikibainika kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya vitendo vya ukatili na matumizi ya pombe kupita kiasi.
Bi. Soka alisema takwimu zinaonesha kuwa wanawake ambao waume zao wanalewa mara kwa mara wengi wao wanakumbana na ukatili unaohusisha vipigo, kuumizwa na ukatili wa kingono kwa asilimia 77, huku kiwango cha ukatili kwa wanawake ambao waume ama wenzi wao hawanywi pombe ni asilimia 33.
"...Utafiti uliofanywa na shirika la IOGT International unaonyesha kwamba kiwango cha unywaji pombe katika jiji la Dar es Salaam ni asilimia 47.6 kwa wanaume na asilimia 29 kwa wanawake...lakini takwimu kutokana na utafiti wa Demographia na Afya Tanzania (TDHS) 2010...unaonesha wanawake ambao waume zao wanalewa mara kwa mara wengi wao wanakumbana na ukatili unaohusisha kipigo/kuumizwa na ukatili wa kingono kwa asilimia 77," alisema.
Aidha aliviomba vyombo vya habari kushirikiana na TAMWA kutoa elimu kwa jamii kupunguza matumizi ya pombe kupindukia kwani licha ya ukatili huo familia pia zimekuwa zikiathirika kiuchumi juu ya matumizi ya pombe huku baadhi ya watoto wakikosa huduma za msingi kutoka kwa baadhi ya wazazi ambao ni walevi kupindukia.