MAHAKAMA ya Afrika inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu, jana imetoa hukumu katika kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila, ambayo italazimisha kusitishwa kwa Bunge la Katiba ili kupisha utekelezaji wa sehemu ya hukumu hiyo ambayo ni ya kikatiba.
Katika hukumu hiyo, mahakama imeitaka serikali kutekeleza kwa vitendo hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Juni 14, mwaka jana katika kesi ya kudai mgombea binafsi katika uchaguzi wa ngazi zote, iliyofunguliwa na Mchungaji Mtikila dhidi ya serikali.
Akisoma hukumu hiyo, Rais wa majaji wa mahakama hiyo, Jaji Sophia Akuffor, mbele ya wawakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alitaka serikali ndani ya miezi sita kwanza kutangaza katika gazeti la serikali hukumu iliyompa ushindi Mchungaji Mtikila ya mgombea binafsi na pia kutangaza hukumu hiyo katika wavuti ya serikali.
Jaji huyo aliitaka serikali kuwasilisha katika mahakama hiyo utekelezaji wa hukumu hiyo na kubainisha kuwa imeweka katika mchakato suala la mgombea binafsi ili kutekeleza hukumu hiyo.
Alisema pia katika matangazo hayo, hukumu hiyo iwe imetafsiriwa katika lugha nyepesi ya Kiswahili na Kiingereza ili kuwawezesha wananchi wote kuisoma vizuri.
Hukumu hiyo imeipa serikali miezi tisa iwe imewasilisha kwa maandishi na vielelezo vya kuonyesha imetekelezaje hukumu hiyo ya jana na vipengele vyake vyote vya hukumu.
Mbali ya kuishindilia serikali katika hukumu hiyo, Jaji Akuffor alitupilia mbali madai ya Mchungaji Mtikila katika kesi yake ya msingi namba 011 ya mwaka 2013 ya kutaka kulipwa fidia za gharama za kesi kwa wanasheria wake, gharama za yeye kupewa manyanyaso na serikali akidai haki hiyo kabla ya kufungua kesi hiyo ya kihistoria, na pia gharama alizotumia katika mchakato mzima wa kesi yake ya awali ya kudai mgombea binafsi ambayo alishinda.
Katika msingi wa kesi hiyo ya madai, Mtikila alitaka kulipwa zaidi ya sh bilioni 9 za gharama zote kwa kushinda kesi ya awali, madai ambayo mahakama hiyo baada ya kuyapitia, ilikosa vielelezo vya kuyathibitisha.
Akitupilia mbali madai ya Mtikila kunyanyasika kibinadamu kwa kukosa haki yake ya mgombea binafsi, Jaji Akuffor alifafanua kuwa kwa hukumu iliyotolewa mwaka jana na kumpa ushindi, ilitosha kufidia machungu aliyoyapata katika kuikosa haki hiyo.
Awali Mtikila alipinga mwananchi wa Tanzania kulazimishwa kujiunga na chama cha siasa ndipo apate sifa ya kuwa mgombea katika chaguzi mbalimbali za kisiasa, ikiwemo urais, ubunge na udiwani.
Akizungumza nje ya mahakama baada ya ushindi huo, Mchungaji Mtikila alisema hukumu hiyo ni ushindi mkubwa kwa Watanganyika wote kwani kuanzia sasa watakuwa na nafasi ya kumchagua mtu wanayemuona anawafaa kuwaongoza bila kujali siasa za vyama.
Alisema kwa hukumu hiyo, ni wazi hakuna uwezekano wa kuendelea kwa mchakato wa Bunge la Katiba hadi pale vipengele vya mgombea binafsi vitakapowekwa katika rasimu ya katiba mpya.
“Baada ya hukumu hii, siku chache zijazo naleta tena maombi mapya ya kufutilia mbali Bunge la Katiba kwa kuwa limekiuka katiba ya nchi kwa wajumbe wake kuteuliwa na mtu mmoja kwa maslahi ya kikundi cha watu wachache,” alisema Mtikila.
Alifafanua kuwa katika kesi hiyo ataitaka mahakama iilazimishe serikali kuwaachia wananchi wajitengenezee katiba yao badala ya sasa kutengenezewa katiba na watu wachache, tena wote wakiwa wanasiasa kwa maslahi yao ya kisiasa.
“Jamani wote mnashuhudia jinsi wajumbe waliochaguliwa na mtu kuingia katika Bunge hilo la katiba wengine wakiwa hawana sifa na ambao tutawataja kwa majina wakati ukifika, ambao kazi yao katika Bunge lile ni kuzomea watu tu,” alisema Mtikila.
Akinukuu baadhi ya maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Mtikila alisema muasisi huyo katika mambo ya msingi ambayo aliona kwa wakati huo bado Watanzania hawana uwelewa nayo wa kutosha, aliyaacha ili kutoa muda kwa wananchi wake wajifunze kwanza.
Mawakili wa serikali waliokuwepo mahakamani hapo, walikataa kuzungumzia hukumu hiyo kwa madai kuwa wao sio wasemaji wa idara hiyo.