AWALI sikuamini, hadi nilipohakikishiwa kuwa picha za umati wa Watanzania wenzetu, 10,800 hadi 10,900 ni kweli walikusanyika katika Uwanja wa Taifa, kwa ajili ya kusaka nafasi 70 za ajira kutoka Uhamiaji.
Ndio, maana nilitegemea kuwa umati ule ungepigwa katika mikutano ya kisiasa au matukio ya mpira wa miguu, hususan Simba, Yanga au timu ya Taifa (Taifa Stars). Lakini sivyo. Uamuzi wangu wa kumpigia simu swahiba au kijana mwenzangu aliyekuwa miongoni mwa watu hao waliokwenda kufanyiwa usaili ulikuwa wa muhimu.
Alinijibu, “Ni kweli picha hizo ni za waliokwenda kufanyiwa usaili wa nafasi 70 za Uhamiaji, nzuri zaidi na mimi nilikuwapo hapo uwanjani Juni 13, mwaka 2014,” alijibu. Maneno haya yalinikera. Yalinikera nikiamini kuwa hakukuwa na ulazima wa kuitwa watu wote hao kufanyiwa usaili.
Huu ni udhalilishaji wa wazi wazi kwa Watanzania wenzetu. Ikiwa wanaohitajika ni watu 70, sitaki kuamini kuwa wahusika wangeshindwa kuwachagua kulingana na mahitaji yao. Pengine ingekuwa nzuri zaidi kuchagua watu 200 na kuwachuja katika siku hiyo ya usaili.
Uhamiaji walikwenda kujua nini? Sifa gani wanazohitaji kutoka kwa Watanzania hawa 10,800 waliozagaa katika Uwanja wa Taifa? Naogopa. Mtizamo wa waliokuwa katika nafasi nzuri serikalini wanajua wenyewe.
Na ndio maana mchakato huu unaidhalilisha serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sikatai kuwa ajira ni tatizo kubwa. Watanzania wengi hawana ajira kwasababu ya kufa kwa viwanda vyetu. Pia baadhi yao wanaona kuajiriwa ndio suluhisho ya matatizo yao.
Kwa bahati mbaya, huenda pia suluhisho halijulikani, ikiwamo kuwaandaa vijana kusoma kozi kulingana na soko la ajira au hata kuwawezesha kwa mtindo mwingine, kama vile biashara, kilimo au mengineyo muhimu.
Vijana hawa hawajaandaliwa kujiajiri bali kuajiriwa. Inapotokea nafasi za kazi, utaona mahitaji ni watu 10 lakini waombaji kazi makumi kwa mamia. Hivyo basi; badala ya kuwajaza kama walivyofanyiwa hawa, ni bora utaratibu ni wengi. Kwa mwaka wanaoingia kwenye soko la ajira ni wengi kutokana na vyuo vingi kuzalisha makundi kwa makundi. Wingi wa watu hao hauendi sambamba na wingi wa nafasi za ajira serikalini na sekta binafsi pia.
Hivyo utaratibu huu ungekuwa wa kuwachagua kulingana na sifa na mahitaji husika kabla ya kuitwa kwa idadi kubwa isiyolingana na mahitaji yao. Narudia tena, hakukuwa na ulazima wowote wa kuwajaza uwanjani Watanzania hawa.
Huku ni kuwavunja moyo. Ni kuwapandikizia sumu dhidi ya serikali yao. Wakitoka pale, watatoka na picha moja kubwa. Picha ya serikali kuwanyima ajira. Nani ametoa uamuzi huo wa kuwachoma na jua nguvu kazi hii ya Taifa?
Baadhi ya mambo yanavyofanyika yanazalisha chuki kwa serikali hii ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Rais ambaye umakini wake, utukufu wake na uchapakazi wake unatatizwa na watu anaowaamini wasimamie baadhi ya mambo serikalini.
Hii si haki hata kidogo. Hivi kweli tunajivunia elimu zetu wakati zinashindwa kutambua baya na zuri kwa manufaa ya nchi yetu? Au tunawapa watu maneno ya kusema? Kwamba watu wajuwe nchi hii ina janga kubwa la ajira?
Hebu tujiulize, inapotokea tatizo la mripuko au janga lolote kwa tukio hilo la usaili wa nafasi chache za ajira nani wa kumlaumu? Narudia tena, nimeumizwa na kuchukizwa. Waliopendekeza usaili ufanyike kwa siku moja, muda mmoja ni nani? Aibu.
Hii ni aibu na pengine walitaka iingie kwenye kumbukumbu za Kidunia. Saa chache baada ya kufika kwenye usaili huo, mitandao ya kijamii ilipendeza picha hizo. Kila mtu alisema lake, wakiwapo wale walioisema vibaya serikali.
Mbaya zaidi, wapo wanaoamini kuwa waliokwenda kufanyiwa usaili si wale watakaopewa ajira hizo kutokana na sababu wanazosema wao. Hii inaonyesha ni jinsi gani watu wanavyokosa imani na Watanzania wenzetu.
Sawa, fikiria mtu aliyechomwa na jua katika usaili huo kisha ajira yenyewe anakosa. Nini afanye mtu huyu? Nani wa kumfariji? Ndio, anaweza kuona ushindani ulikuwapo, lakini kwanini watu hao makundi kwa makundi wasingeganywa?
Au hata kuwachuja kama nilivyosema hapo juu?
Hii haiwezekani. Kila mmoja lazima afanye kazi kwa bidii pamoja na kuweka sawa fikra sahihi kabla ya kuamua lolote. Tabia hii ya kuwakusanya Watanzania wenzetu kwa kisingizio cha usaili wa nafasi za kazi zikome mara moja.
Watafutiwe utaratibu mwingine mzuri. Huu ni udhalilishaji, ingawa huenda wengine wanaona kawaida. Nasema haya kama Mtanzania, maana tukio hili limefanyika katika ardhi ya nchi yangu na waliokwenda kwenye usaili huo ni Watanzania wenzangu.
Nimekerwa na kuchukizwa, nikiamini kuwa si wote wataipata kazi hiyo ya Uhamiaji. Kweli?
ANGALIZO; Maneno haya ni mtazamo wangu binafsi. Si msimamo wa Taasisi ya Handeni Kwetu Foundation.
Kwa maoni na ushauri
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949