Quantcast
Channel: HABARI NA MATUKIO
Viewing all articles
Browse latest Browse all 19575

TIGO YASHIRIKIANA NA DTBI NA COSTECH KATIKA KUKUZA TEKNOHAMA NA AJIRA KWA VIJANA NCHINI

$
0
0
Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Bw. Diego Gutierrez (wa pili kulia) akipongezana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Dar Teknohama Business Incubator (DTBi) Engineer George Mulamula mara baada ya kutiliana saini ya ushirikiano ambapo Tigo itawawezesha washiriki wa teknohama wa DTBi kuendeleza vipaji vyao kupitia mpango maalum wa mafunzo na biashara ambayo itasaidia kukuza ajira nchini kupitia taaluma ya teknohama. Kushoto ni Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia Profesa Makame Mnyaa Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dk. Hassan Mshinda.
Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Bw. Diego Gutierrez (kulia) akitiliana saini na Afisa Mtendaji Mkuu wa Dar Teknohama Business Incubator (DTBi) Eng. George Mulamula kama ishara ya ushirikiano kati ya Tigo na kituo hicho cha biashara ya teknohama DTBi. Wanaoshuhudia kutoka nyuma ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dk. Hassan Mshinda. Tigo itatoa nafasi ya kuwasomesha watanzania 10 katika ngazi ya Shahada ya Uzamili kila mwaka.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Bw. Diego Gutierrez (kushoto) wakimsikiliza kwa makini mmoja wa washiriki wa mpango maalum wa Tigo na DTBi katika kukuza vipaji vya teknohama Bw. Godfrey Magila ambaye ameweza kubuni programu ya kuangalia vipindi vya Bunge kupitia simu za mkononi za kisasa. Tigo pia itatoa fursa za mafunzo kwa vitendo na nafasi za ajira kwa wale ambao wamejikita katika masomo ya Teknohama.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari na wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya utiliaji saini kati ya kampuni ya Tigo na kituo cha biashara ya teknohama DTBi. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Bw. Diego Gutierrez na Afisa Mtendaji Mkuu wa DTBi Eng. George Mulamula
---
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Tigo Tanzania imeingia katika ushirikiano na Dar Teknohama Business Incubator (DTBi) ambayo itaona kampuni hiyo ya simu ikiwezesha washiriki wa teknohama kukuza vipaji vyao kupitia mpango maalum wa mafunzo na biashara ambayo itasaidia kukuza ajira nchini kupitia taaluma hii ya teknohama.

Akizungumza kuhusu ushirikiano huo katika makao makuu ya Tume ya Sayansi na Teknolojia jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Tanzania Bw. Diego Gutierrez alisema kwamba ushirikiano huo na DTBi utawapatia watanzania ambao ni wanasayansi wa baadaye fursa ya kujifunza na kuendeleza vipaji vyao huku biashara inayotokana na teknohama ikizidi kukua na kuchangia suluhu za kidigitali katika jamii.

“Hadi sasa teknohama inachangia asilimia 2.3 katika GDP ya nchi, Tigo ina dhamira ya dhati katika kuhakikisha kiwango hiki kinakua kupitia uwekezaji wa rasilimali watu. Ni kwa sababu hii kupitia Dar Teknohama Business Incubator (DTBi) Tigo pia tunatoa ahadi kuwasomesha watanzania 10 katika ngazi ya Shahada ya Uzamili kila mwaka, pamoja na kutoa nafasi ya mafunzo na nafasi za ajira kwa wale ambao wamejikita katika masomo ya Teknohama,” Gutierrez alisema.

Gutierrez aliongeza, “Hii inaendana barabara na Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ya mwaka 2015 na sera ya Tanzania ya Teknohama ya mwaka 2013 katika kuongeza upeo wa ufahamu wa masuala ya teknohama katika jamii ya watanzania. Kwahiyo tunafuraha ya kuungana na serikali ili kutoa mchango wetu katika kufanikisha hili.

Utiaji saini wa ushirikiano huu ulishuhudiwa na Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia Professa Makame Mbarawa ambaye aliipongeza Tigo na DTBi kwa kuingia katika ushirikiano huo. Alisema, “Serikali inayo furaha kubwa sana kuwaunga mkono katika ushirikiano huu ambayo utaendelea kuwawezesha vijana na wajasiriliamali wa teknohama kupata maarifa na msaada katika kukuza ubunifu wao ili kuweza kushindana kikamilifu katika soko la biashara siku za usoni.”

“Tunaamini ya kwamba ushirikiano huu hautatoa fursa ya ajira tu kwa vijana wetu kuonyesha ubunifu wao bali utawawezesha pia kuweza kujipatia kipato na kupanua wigo wa aina za biashara zitakazoweza kufanyika hivyo kuwezesha ukuaji wa kasi wa maendeleo ya kiuchumi na kifedha katika jamii yetu. Napenda kuipongeza Tigo, DTBi na COSTECH kwa ushirikiano wao huu ambao utakuza teknolojia na kutengeneza thamani kubwa ya biashara za aina yake kwa vijana,” alisema Mbarawa.

Akizungumza katika uzinduzi wa ushirikiano huo Afisa Mtendaji Mkuu wa DTBi Engineer George Mulamula alisema kwamba ushirikiano huu utawapa washiriki fursa mbalimbali kuonyesha vipaji vyao kitaifa na kimataifa.

“DTBi inalenga katika kutengeneza utamaduni wa ujasiriamali wa teknohama pamoja na kuongeza ajira katika wigo wa ubunifu wa teknolojia. Tuligundua ya kwamba washiriki wetu walikuwa wanakosa uzoefu wa kutosha pamoja na uzoefu wa mazingira ya kufanya biashara ambao ungewawezesha kuwafanya kuwa wajasiriamali bora zaidi. Kwahiyo tuna matumaini makubwa ya kwamba Tigo watatusaidia kutatua tatizo hili,” alisema Engineer Mulamula.

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dk. Hassan Mshinda pia alisema kwamba ushirikiano huu kati ya Tigo na DTBi unaenda sambamba na dira ya tume hiyo katika kuendeleza uchumi wa taifa kupitia ukuaji wa maarifa, utafiti na maendeleo ya teknolojia pamoja na ubunifu kwa ajili ya maendeleo nchini Tanzania. Aliongeza, “Tigo inawapa fursa ya kipekee washiriki wetu wa teknohama katika kutimiza ndoto zao.”

“Kupitia ushirikiano kama huu wa kidigitali tunaweza tukafanya kazi na sekta binafsi kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi huku tukikuza kiwango cha teknohama na maarifa yake kwa wadau mbalimbali nchini,” alisema Dk. Mshinda. “Pia ni namna ya kuonyesha kwamba kupitia ubunifu unaotokana na sayansi na teknolojia tunaweza pia kuendeleza ufanyaji biashara ambao utatoa matokeo chanya katika uchumi wetu pamoja na kutuongezea nafasi za ajira nchini. ”

Viewing all articles
Browse latest Browse all 19575

Trending Articles