




MTANDAO Mtandao wa Mashirika Huru ya Kijamii (CSOs) nchini Tanzania pamoja na baadhi ya wanafunzi wa kike shule kadhaa za Sekondari jijini Dar es Salaam umefanya maandamano kupinga kitendo cha kikatili kilichofanywa na kikundi cha Boko Haram cha nchini Nigeri cha kuwateka wanafunzi wa kike na kuwashikilia.
Maandamano hayo ya ndani yaliyoshirikisha wanaharakati mbalimbali yamefanyika ndani ya viwanja vya TGNP Mtandao eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi wa mashirika yanayounda CSOs walipokea maandamano na kusoma barua maalumu yenye ujumbe wa kupinga utekaji uliofanyika na kuishinikiza Serikali ya Nigeria itekeleze matakwa ya watekaji ili wanafunzi waliotekwa waachiwe huru.
Akisoma barua hiyo kwa niaba ya CSOs, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi alisema mashirika yao yanaotetea haki za wanawake na watoto yameamua kuungana na mitandao na wanaharakati wengine duniani kote kulaani kitendo cha kinyama cha kuwateka nyara wasichana wanafunzi zaidi ya 200 waliokuwa shuleni nchini Nigeria, tukio lililofanywa na wanamgambo wa kikundi cha Boko Haram.
Alisema mashirika hayo yametumia maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia ulimwenguni kulaani kitendo hicho cha kikatili na kuitaka Serikali ya Nigeria kuhakikisha inawajibikaji ipasavyo ili kuwarejesha mateka hao mara moja tena wakiwa salama.
CSOs wamelazimika kufanya maandamano hayo ya ndani baada yale ya kutaka kuandamana hadi Ubalozi wa Nigeria kuzuiwa na Jeshi la Polisi kwa sababu kadhaa. Hata hivyo baadhi ya askari polisi walikuwa pembeni mwa viwanja vya TGNP Mtandao katika huku zoezi la maandamano ya ndani likiendelea. Baadhi ya Mashirika yanayounda CSOs ni pamoja na TAMWA, TGNP Mtandao, WiLDAF, LHRC.