Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Bachelor of Insurance and Risk Management katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) amezama na kupotelea baharini alipokuwa katika Pantoni akivuka akielekea Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza na Kajunason Blog mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa mwanafunzi huyo alikuwa akivuka na wenzake jioni ya leo kuelekea Kigamboni jijini Dar mara baada ya kutoka kwenye mtihani wake ndipo alipokutwa na mauti hapo.
Sakata hilo lilianza mara baada tu ya Pantoni hilo kukaribia eneo la kivuko cha Kigamboni ndipo mwanafunzi huyo alipoanza kubishano na wanafunzi wenzake kuwa anauwezo wa kuzamia na kupiga mbizi, katika kuwahakikishia hilo alivua viatu pamoja na shati lake na kuwapatia wenzake na kujitosa kwenye maji ili apige mbizi kuwahakikishia wenzake uhodari wake.
"Kiukweli ni jambo la kushangaza sana, ulitokea ubishani wa wanafunzi baada ya mwenzetu huyu kuwa anajisifia kuwa anajua kupiga mbizi ndipo alipovua viatu na shati na kujitosa kwenye maji, kwa bahati mbaya aliangukia upande wa Pantoni lilipokuwa likipiga makasia na kwa kawaida sehemu hiyo maji huwa yanakasi sana hivyo yalimsababishia mwanafunzi huyo kushindwa kuibuka na kumfanya azame katika kina kirefu,"
Mpaka sasa mwanafunzi huyo bado hajaonekana... Juhudi za kumtafuta bado zinaendelea.