Mdhamini Mkuu wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, wameipongeza timu ya Azam FC kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa 2013/2014 ikiwa ni Mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake miaka 7 iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mechi kati ya Mbeya City na Azam FC kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya sokoine mjini Mbeya Meneja Uhusiano wa Nje wa Kampumi hiyo, Salum Mwalim amesema wakiwa wadhamini wameridhishwa na kiwango cha Azam FC pamoja na timu zote zinazoshiriki katika ligi na hivyo wanawapongeza kwa dhati timu hiyo kwa kuibuka mabingwa.
"Tunachukua nafasi hii kuwapongeza Azam kwa kuwa bingwa mpya wa Vodacom Premier League (VPL) 2013/2014, wamekabiliana vema na mikikimikiki ya ligi na hivyo ubingwa wao haukuwa mwepesi kuupata kutokana na ushindani uliokuwepo kwa timu zote shiriki"Alisema Mwalim
"Tumeifuatilia ligi na tunaimani kuwa Ligi imetoa bingwa aliyestahili na ambae yupo imara kutokana na kupitia safari ndefu na ngumu ya ligi na ni imani yetu kwamba atakuwa mwakilishi mzuri kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika akiitangaza nchi na pia Vodacom Premier League."Alisema
Mwalim amesema Azam inabeba kwa mara ya kwanza ubingwa wa ligi tangu timu hiyo ilipoanza kushiriki ligi kuu mmwaka 2008 na kwamba ushindi huo bila shaka utaongeza ushindani kwenye msimu ujao.
"Ubingwa wao huenda ukaifanya ligi ya mwakani kuwa ngumu zaidi kwani timu za Yanga na Simba ambazo zimekuwa zikipokezana ubingwa kwa takribani miaka 20 zitataka kurudisha heshima yao na nyengine zikipata nguvu kuwa yoyote anaweza kuwa bingwa iwapo atajipanga vema kumudu ushindani,hilo likitokea ubora wa ligi yetu utazidi kupaa"Alisema Mwalim
Amesema Azam watakabidhiwa kombe lao la ubingwa April 19 kwenye uwanja wa nyumbani Chamazi wakati wa mechi yao ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu.
Akizungumzia ligi, Mwalim amesema ilikuwa ya ushindani mkubwa na takribani kila mechi ilikuwa ngumu kwa kila timu hali iliyolazimisha hata bingwa kujulikana kwenye mechi za mzunguko wa mwishoni.
"Tumefika mahali tunapoweza kuzungumza mazuri zaidi kuhusu ligi tofauti na tulikotoka,ni wazi kwamba ligi yetu imepiga hatua na Vodacom kama mdhamini Mkuu tutaendelea kufanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kuimarisha ubora huo."Alisema Mwalim
Aidha Mwalim amezipongeza timu zote 14 zilizoshiriki ligi hiyo kwa kujituma na kutoa changamoto katika kila mechi jambo lililofanya bingwa kutopatikana kwa urahisi na mapema.
Aidha amezipongeza timu za Yanga na Mbeya City kwa kuwa katika msimamo wa kumaliza kwenye nafsi ya pili na ya tatu huku akiitaja timu ya Mbeya City kuwa ni timu iliyoleta changamoto mpya kwenye ligi na kuipa afya zaidi ligi hiyo.
"Mbeya City wamecheza vizuri sana tangu mwanzoni mwa ligi hadi wanapoelekea kumaliza mchezo wao wa mwisho wa ligi,wameonesha mfano kwa timu zinazopanda daraja nanmna gani wanavyoweza kuwa timu shindani badala ya kuwa timu shiriki."Aliongeza Mwalim
Alisema awali ilionekana kuwa ni nguvu ya soda lakini kadiri ligi ilivyokuwa ikosonga mbele ilionesha kuwa imedhamiria kufanya vema huku ikihimili mikikimiki yote ya ligi kuu na hivyo kuifanya kuwa timu inayohitaji kupewa sifa za kipekee kwa msimu huu.
Vodacom imewapongeza pia wakazi na wenyeji wa mkoa wa Mbeya kwa kuiunga mkono timu yao kwa hali na mali na hivyo kuipatia mafanikio huku hatua yao hiyo ikinogesha pia joto la ligi ndani na nje ya mkoa wa Mbeya.