Wasafiri wa safari ziendazo mikoani leo wamejikuta katika wakati mgumu baada ya safari zao kuishia kituo cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo jijini Dar kutokana na foleni iliyopo daraja la Ruvu iliyosababishwa kujaa kwa maji.
Wakizungumza na Kajunason Blog kwa nyakati tofauti baadhi ya wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani walisema kuwa hali tete iliyopo katika daraja la Ruvu mkoani Pwani iliyosababishwa na mvua nyingi ndiyo iliyosababisha kukwama kwa safari za mikoani.
Walisema maji mengi na barabara imemeguka upande wa darajani hapo imekuwa chanzo kikuu cha kusababisha msongamano mkubwa wa magari ya abiria na mizigo yaliyokuwa yanaingia na kutoka mkoani Dar es salaam, hivyo kupelekea safari za leo kuahirishwa kusubiri matengenezo na njia mbadala kupatikana.
Aidha wameongeza kuwa hakuna namna yoyote wanayoweza kufanya zaidi ya kubadilisha tarehe za safari na kusubiri tamko la serikali kuhusu kufunguliwa kwa njia hiyo.
Kajunason Blog ilienda mbali zaidi na kuzungumza na baadhi ya wasafiri ambao walikuwa wamebaki na hali ya sintofahamu ya uhakika wa safari huku wakiwa wamekata tama.
Wamesema kuwa miundo mbinu mibovu ya barabara ndio chanzo kikuu cha kero hii japo mvua ni Baraka ila ikizidi huleta maafa.