TAMKO LA KATIBU MKUU KIONGOZI KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU HATI YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR
IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 14 APRILI, 2014
______________________________________________
Siku 12 zijazo tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar, na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wamezaliwa watu ndani ya Muungano huu na wengine wana wajukuu.
Inasikitisha sana kuwa leo, miaka 50 baadaye ipo dhana
potofu inayojengwa kuwa Muungano huu si halali kwa vile hakuna Hati ya
Muungano (Articles of the Union).
Waasisi wa Taifa letu ambao tarehe 22 Aprili, 1964 kule
Zanzibar walitia saini Hati hiyo, mbele ya mashuhuda, nao wameonekana
kama walichokifanya kilikuwa kiini macho, na kwa hiyo kwamba waliongoza
Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msingi wa kiini macho
hicho kwa miaka yote hadi Mwenyezi Mungu alipowaita.
Mambo yote mawili yametusononesha sana sisi Serikalini, na
bila shaka yamewasononesha wananchi wanaoipenda nchi yao, wanaowapenda
Waasisi wa Taifa letu na kuuenzi Muungano wao.
Madai ya kuonyeshwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi
lakini hatukuweza kuamini hali itafikiwa ilipofikia, ambapo wapo watu
wanathubutu kudai na kuapa kuwa Hati hiyo haipo.
Ukweli ni kuwa hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote. Hata
hivyo, lazima tukubaliane kuwa zipo Hati fulani ambazo ni kiini cha
uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru, ambazo
tunazihifadhi kama mboni ya jicho. Hati hizo ni pamoja na Hati ya Uhuru
wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962,
na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964. Hati za
aina hii zinahifadhiwa maeneo maalum ambayo ni salama ili zisipotee wala
kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi, tunazifungua ili kuzihifadhi kwa
namna yoyote ile.
Lakini sasa maneno yanakua mengi, tuhuma zimekuwa nyingi,
dhihaka zimekuwa nyingi, kiasi cha wananchi kuanza kutiwa mashaka iwapo
kweli Hati ya Muungano ipo au la.
Hivyo, kwa maagizo na ridhaa ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninaleta mbele
yenu Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar
na waasisi wetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman
Karume, ili muione na kuwahakikishia Watanzania kuwa yanayosemwa kuwa
hakuna Hati hiyo si kweli. Hati hiyo ipo tangu wakati huo, imetunzwa
vizuri na waliotutangulia, tumeirithi, na tutaendelea kuihifadhi.
Na, tukiombwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge Maalum
nina uhakika Rais ataridhia ipelekwe huko ili kuondoa mjadala wa kama
Hati ipo au la.
Isitoshe, tufanye utaratibu wa kuweka nakala kwenye
Makumbusho ya Taifa ili kila atakayetaka kuiona katika miaka mingine 50
ijayo na kuzidi aione.
Mwisho, narejea kusema kuwa kwa upande wa Serikali
tunasikitishwa na kufadhaishwa sana na tuhuma nzito kwamba labda waasisi
wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini macho. Hatukutarajia wawepo
Watanzania wenzetu, wafikie hapo.
Ni jambo zito. Vile vile hatukutarajia kuwa Serikali
itatuhumiwa kuwa haikuwa makini kuhifadhi waliosaini waasisi wetu.
Matumaini yetu ni kuwa baada ya leo tutaendelea na mambo ya
msingi kwa mustakabali, umoja na uimara wa Taifa letu badala ya
kuchochea hisia kuwa Muungano wetu hauna msingi imara wa kisheria.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
14 Aprili, 2014