Fikra za kila mtu hazijifichi, matokeo yake huleta tabia, tabia huleta matokeo hasi ama chanya.
Fikra ni sawa na mbegu ndani ya maisha yetu... Unapopanda mbegu kwenye udongo, matokeo yake huota kile ulichokipanda, kama umepanda mahindi, utavuna mahindi. Vivyo hivyo, jinsi unavyofikiri (unavyowaza), unapanda mbegu katika mitazamo na mienendo ya maisha yako na matokeo yake huonekana sawia na fikra zako.
Ni wazi kuwa huwezi kupanda mahindi ukavuna machungwa, vivyo hivyo huwezi kupanda mbegu itokanayo na fikra za kushindwa, umasikini, huzuni, kisha ukapata matokeo ya maisha mazuri, furaha na amani. Hivyo ni wazi kuwa ukitaka jambo jema litokee, anza kupanda kwanza fikra za wema (jambo hilo). Ukitaka kupata matokeo mazuri katika mahusiano anza kwanza kupanda mbegu ya mtazamo chanya juu ya mahusiano, upendo na furaha. Kama matarajio yako ni kuona dunia yenye mazingira mazuri na bora kwa viumbe wote, anza kwanza kupanda fikra ya wema na kujali viumbe wengine. Ukitaraji kuona mwenzi wako ana mwenendo mwema, anza kupanda mbegu ya ushirikiano, upendo, kujali badala ya kufikiri kuwa kuna jambo nje yako wewe, ama nguvu nje yako itakayoleta mabadiliko maishani mwako. Fikiri vema juu yako ubadili maisha yako. Muonekao wa mazingira yanayotuzunguka ni matokeo ya fikra zetu wenyewe.
Mawazo uwazayo juu yako ni kipimo unachojipimia katika mwenendo na matokeo ya maisha yako. Matokeo yake kamwe hayajifichi. Hatuchagui moja kwa moja juu ya mtiririko wa maisha yetu, lakini kupitia fikra, tunachagua matokeo ya maisha yetu na kuujenga mtiririko wa maisha yetu.
Mazingira huchangia sana binadamu kuwa na fikra Fulani juu (dhidi) yake. Mfano, mtu aishiye katika mazingira ambayo ni ya kipato cha juu, fikra zake huwa mara nyingi si za kushindwa jambo tofauti na aliye katika mazingira yenye vikwazo vingi. Anayepita kwenye magumu mengi, anapojitambua huweza kufanya mambo makubwa kuliko aliyeko kwenye mazingira yasiyo na vikwazo vingi kwa sababu huanza kuwa na fikra za ushindi.
Tunapofikiri hasi juu ya maisha yetu, tunapata matokeo hayohayo. Tunapofikiri chanya na kuchukulia kila jambo ama mazingira kama nafasi, matokeo yake ni kukua zaidi na kusonga mbele. Tunachokipata maishani ni matokeo yenye uasilia ndani mwetu na si nje yetu. Tabia za marafiki ulionao ni picha ya tabia ulionayo wewe. Matokeo ya mafanikio ama kutofanikiwa kwa wewe na unaowaongoza ni picha ya fikra ulizonazo pamoja na unaowaongoza.
Ukijitazama kwenye kioo, unaiona sura yako. Kama una makovu, si tatizo la kioo, ni uhalisia wa jinsi ulivyo. Tabia unazoonesha nje, ni picha halisi ya fikra zako ndani mwako.
Unaweza kujifunza fikra, tabia na mienendo ya jamii kwa kuangalia matokeo yake. Jamii yenye umasikini, maradhi na ujinga ni picha halisi ya fikra zao, elimu yao na mitazamo yao. Ukiona katika jamii wapo watu wanaopenda kutembea wakiwa nusu uchi, ni picha kamili kuwa wengi wa wana jamii hiyo wanapenda tabia hiyo. Mbuzi hawezi kuzaa kondoo, na kinyume chake ni sawia.
Wapo wanaodhani kuwa fikra alizonazo mtu huweza kuwa siri. Ukweli ni kwamba matokeo ya matendo yako, ni matokeo ya mawazo yako. Fikra zetu huonesha matokeo sawasawa na msukumo wake. Anayefikiri dunia ni sehemu mbaya, huishi akiishutumu dunia siku zote. Anayefikiri watu wanaomzunguka ni kikwazo kwake, huishi daima ikawaona kuwa ndio sababu ya matatizo yake. Fikra huonekana matokeo yake haraka kwenye tabia na tabia huleta matokeo ya maumivu ama furaha (majuto ama furaha). Kwa kifupi tabia uliyonayo, iletayo matokeo yake ya majuto ama furaha ndiyo inayotoa picha ya fikra iliyotoa msukumo wa matokeo hayo.
Fikra yenye woga, wasiwasi na kutowajibika huonesha tabia ya unyonge, kutojiamini na kutochukua hatua, matokeo yake ni kukata tamaa, kushindwa na kuwa tegemezi kwa kila jambo.
Nazo fikra yenye uvivu hupelekea tabia za udhaifu/unyonge, udanganyifu (usanii sanii) na matokeo yake ni kuwa ombaomba, masikini na uzembe. (ukiona nchi ina kila rasilimali, na inakuwa masikini, basi ujue watu wake wote ni wavivu kufikiri na wasipobadili fikra hizo watabaki kuwa ombaomba hata kama matrilioni ya pesa yatatolewa kama msaada)
Fikra za chuki na kutojiamini huleta tabia za visasi na uonevu, matokeo yake ni vurugu, kutoweka kwa amani, mauaji ya kutumia nguvu. Unaweza kujifunza matokeo ya viongozi wasiojiamini na wenye chuki.
Fikra za ubinafsi (umimi) huleta tabia ya ushindani, unyang’anyi, (roho mbaya tunaita waswahili). Na matokeo yake kila mmoja anayajua.
Kwa upande mwingine fikra zote njema huleta matokeo mema kwa watu wote.
Fikra za kutia moyo, kujiamini na kuchukua hatua huonekana katika tabia za utu wema na kuwajibika, matokeo yake ni amani, mafanikio na uhuru wa kweli.
Huwezi kuwa huru mpaka utakapokuwa na fikra huru.Ukifahamu jinsi unavyoweza kubadili maisha yako kwa kubadili fikra zako… umeyafikia mafanikio… usikate tamaa.