Na Mwandishi Wetu, Korogwe
SERIKALI imesema itahamisha makaburi na itawaondoa wananchi wote wanaoishi kando kando ya bonde la mto mkomazi kwa kuwalipa fidia za makazi na mimea yao ili kupisha ujenzi wa bwawa kwa ajili kuinua na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.
Rai hiyo ilitolewa jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Jakaya Mrisho Kikwete wakati akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya mamlaka ya mji wa Mombo,Tanga wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo ya wananchi wilayani korogwe.
Rais Kikwete aliyasema hayo mara baada ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Korogwe Lucas Mweri kueleza kwamba serikali ilishatoa kiasi cha shilingi milioni 800 ili kutengeneza mradi huo lakini wananchi walikataa kuondoka katika maeneo hayo kwa madai kwamba ni maeneo yao ya siku nyingi kwa shughuli za kilimo, mifugo, makazi lakini pia katika maeneo hayo yapo makaburi ya ndugu zao.
Rais kikwete aliwaeleza wananchi kuwa hakuna mwananchi mwenye ardhi, Ardhi ni ya serikali na kwamba mwenye mamlaka ya mwisho katika ardhi ni Rais hivyo amesema wananchi hao wataondolewa katika maeneo hayo kwa hali yoyote na gharama yoyote na kwamba hakuna kaburi lolote litakalo tumbukia katika bwawa hilo.
Kikwete alisema makaburi yote yatatafutiwa maeneo maalum kwa kuhamishwa mabaki ya miili na kuzikwa upya kwa imani za kidini za ndugu zao.
Hata hivyo alisema serikali inapotaka kufanya jambo lolote la maendeleo hakuna kikwazo kitakachowekwa na mwananchi yeyote, na kwamba ni lazima serikali iendelee kuelekeza nguvu zake katika kilimo ili wananchi waweze kujikwamua na umaskini.
Rais alisema bonde hilo ni miongoni mwa maeneo yanayoonekana kuwa mkombozi wa maisha ya watanzania hivyo serikali itapeleka nguvu katika eneo hilo ili kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na uhifadhi wa mazingira.