Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametoa shilingi milioni 30 kuchangia mradi endelevu wa kulea na kuhifadhi mbwa mwitu waliokuwa wameanza kutoweka kabisa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.
Mhe. Rais pia amezishukuru na kuzipongeza taasisi za umma na binafsi zinazoshiriki katika kuufanikisha mradi huo unaojulikana kama Vodacom Foundation Serengeti Wild Dogs Conservation Project.
"Juhudi hizi za kurudisha tena makundi ya mbwa mwitu kwenye mbuga hii inayojulikana kimataifa ni ya kupongezwa kwani itahakikisha kwamba wanyama hawa wanaendelea kuwepo Serengeti na pia itaongeza idadi ya vivutio vyetu vya utalii mbugani humu", alisema Mhe. Rais
Aliyasema hayo Jumapili Desemba 23, 2012 wakati wa sherehe za kuachiwa huru kundi la pili lenye mbwa mwitu 15 waliokuwa wamehifadhiwa kwa miezi kadhaa kwenye boma maalumu la mradi huo, lililojengwa katika eneo la Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.
"Nashukuru taasisi zote zinazounga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha kwamba mbwa mwitu wanakuwepo kwa wingi mbugani Serengeti kama ilivyo katika mbuga zingine", aliongezea Mhe. Rais.
Katika taarifa yake wakati wa sherehe hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk. Simon Mduma, alimueleza Rais Kikwete kuwa jumla ya Mbwa mwitu ishirini na sita (26), wamerudishwa mbugani hadi sasa, kufuatia kundi la kwanza la wanyama mwitu hao kumi na moja (11) kuachiwa siku ya Alhamisi Agosti 30, 2012.
Alitanabahisha kwamba mradi huo unaohusisha mbwa mwitu walioondolewa katika msitu wa Samunge wilayani Loliondo ni mojawapo ya juhudi za kurudisha tena makundi ya wanyama hao katika mbuga hiyo maarufu duniani, na kwamba baada ya kuhifadhiwa na hatimaye kuachiwa kwao huku wakiwa wamevishwa collar maalumu zenye redio ili kufuatilia nyendo zao, ni muendelezo wa juhudi za kupata makundi sita yenye mbwa mwitu takriban kumi (10) kila moja, ikiwa ni hatua endelevu ya muda mrefu ya kuhakikisha uwepo wa wanyama hao mbugani humo.
Dkt. Mduma alisema kundi la kwanza la mbwa mwitu hao kumi na moja (11) wote wapo hai na wanaendelea vizuri katika maisha yao mbugani humo, na kwamba pamoja na wanyama hao kutembelea hadi maskani yao ya awali ya Loliondo, malalamiko ya kuwapo kwa uharibifu wa mifugo sehemu hizo kama ilivyokuwa awali hayajaripotiwa hadi sasa.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa utafiti wa wanyama pori alieleza kuwa mbwa mwitu wamekuwa wakitoweka kutokana na kuuawa kwa sumu na wananchi baada ya kula mifugo yao, ama kwa kuugua magonjwa mbalimbali kama vile kichaa cha mbwa.
"Hivi sasa kuna makundi 11 yanayofuatiliwa, manane yakiwa Loliondo na matatu katika Hifadhi ya Ngorongoro, yakifanya idadi ya mbwa mwitu kuwa 200", alisema Dkt Mduma.
Aliongezea kuwa awali, katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti makundi ya mbwa mwitu yalikuwa yakionekana kwa wingi, lakini yamekuwa yakitoweka kwa kasi sana kiasi hata mara ya mwisho ni wanyama mwitu hao wawili tu walioonekana katika mbuga ya Serengeti mnamo mwaka 1998.
Mbwa mwitu ni miongoni mwa wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka duniani.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika Bara la Afrika kuna mbwa mwitu takriban 8,000 na kwamba Tanzania pekee inakadiriwa kuwa na wanyama hao 3,500 katika mbuga mbalimbali nchini, isipokuwa katika Hifadhi h ya Taifa ya Serengeti ambako walianza kutoweka kabisa kabla ya juhudi hizi za kuwarejesha kuanza.
Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom imechangia dola za Marekani 450,000 kwa kipindi cha miaka mitatu ili kufanikisha mradi huo, ambao ulizinduliwa rasmi mwezi Julai mwaka 2011.
"Vodacom tunajisikia furaha sana kuwa sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya utalii ambayo kwa sasa mchango wake ni mkubwa sana kwa taifa", alisema Bw. Salum Mwalimu, Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom wakati wa sherehe za kuwarudisha mbugani mbwa mwitu hao 15.
Bw. Mwalimu alisema kampuni yake siku zote inalenga kubadili maisha ya watu na kwamba ni wazi kuimarika kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inayochangia kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii nchini na ambayo inategemewa kwenye kuongeza pato la Taifa na ustawi wa watu ni jambo muhimu sana.
Taasisi zingine zinazoshiriki katika zoezi hilo ni Idara ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), Frankfurt Zoological Society (FZS) , Grumeti Fund (GF) na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.