Afisa Habari wa Wizara ya Viwanda na Uchukuzi, Nicodemas Mushi (kulia) akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam kuelezea tamko la serikali kuanza ukaguzi wa leseni za biashara. Pembeni yake ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uhamasishaji Biashara na Masoko, Mashingo Christopher.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uhamasishaji Biashara na Masoko, Mashingo Christopher (kati) akikazia tamko la serikali juu ya ukaguzi wa leseni za biashara. Pembeni yake ni Afisa Habari wa Wizara ya Viwanda na Uchukuzi, Nicodemas Mushi (kushoto) na Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo, Frank Mvungi.
Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo.
Serikali ilirejesha utaratibu wa kupata leseni ya biashara kwa kulipia kuanzia 1/7/2013. Wizara ilitoa kipindi cha miezi 6 kwa wafanyabiashara waliokuwa na leseni zisizo na ukomo kuhuisha leseni zao.
Kipindi hicho cha miezi 6 kiliishia 31/12/2013. Na kama tulivyowatangazia Umma, wale waliochelewa kufanya hivyo walipata leseni zao kwa kulipa ada na adhabu kwa mujibu wa Sheria ya Leseni Namba 25 ya 1972 kifungu cha 11(a) na (b).
Ukaguzi: (Kifungu na 17 cha Sheria Na 25 ya 1972)
Ukaguzi unafanyika ili kuhakikisha kuwa biashara zinafanyika kwa mujibu wa Sheria na taratibu za nchi. Kama alivyoagiza KMWVB, kwamba Mamlaka za Leseni zifanye ukaguzi wa kina katika maeneo yao, tunapenda kusisitiza kuwa ukaguzi huu ufanyike kati ya mwezi wa Aprili na Mei.
Wito kwa wananchi
Wananchi kufuata Sheria na taratibu za nchi, kwani kufanya hivyo ni alama ya maendeleo. Kigezo kimoja cha kupima maendeleo ya watu, ni kwa jinsi gani watu hao wanafuata taratibu.