Baadhi ya wananchi wa Namanyere wilayani Nkasi wakichangia damu katika siku ya uzinduzi wa siku ya Utepe mweupe.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Idd Kimanta akiwa na Mkurugenzi wa Evidence for Action, Craig John wakiwa kwenye viwanja vya Sabasaba ambapo mamia ya wananchi walijitolea damu. Mratibu wa Mtandao wa Utepe mweupe, Bi. Rose Mlay akiwapongeza mke na mume waliojitokeza kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wanawake wajawazito.
MTANDAO wa Utepe Mweupe na Uzazi Salama (White Ribbon Allience for Safe Motherhood) umekemea vikali tabia zinazofanywa na baadhi ya watumishi wa hospitali na vituo vya afya ya kuuza damu ambayo kimsingi inatakiwa kutolewa bure kwa wahitaji. Kauli hiyo ya pamoja imetolewa jana wilayani Nkasi na wanaharakati wa mtandao huo walipokuwa katika hafla ya uzinduzi wa wiki ya Utepe Mweupe wilayani hapa, mkoani Rukwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la ‘Evidence for Action’ ambao wanatekeleza mradi ujulikanao kama ‘Mama Ye’, Craig John, alisema wamepata malalamiko toka kwa wananchi ya kuwa kuna tabia ya baadhi ya watendaji kwenye sehemu za kutolea huduma za afya huwauzia wagonjwa damu kitu ambacho hakikubaliki.
“...Wakati tunapita pita mitaani kuhamasisha wananchi kuja kujitolea damu kwa ajili ya akinamama wajawazito wanaohitaji kuongezewa damu, wananchi walituambia kuwa baadhi ya watendaji wa afya wamekuwa kero kwao kwani wanawauzia damu pindi wanapokuwa wanaihitaji,” alisema Craig.
Naye Mratibu wa Utepe Mweupe nchini, Bi. Rose Mlay aliitaka serikali kutenga bajeti mahususi katika mwaka wa fedha 2014/2015 ili kuhakikisha vituo vya afya wanatoa huduma za dharura ikiwemo upasuaji na damu salama.
“...kama mtoto amekaa vibaya tumboni kwa mama au hata kama amepigwa mwanamke huyu anaweza kusaidiwa kwa kufanyiwa upasuaji na kuongezewa damu salama pekee, hivi ndivyo vitakavyo muokoa,” alisema Rose.
Sherehe za kilele cha Wiki ya Utepe Mweupe zinatarajiwa kufanyika Machi 15, 2014 wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda.