Mgeni rasmi Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Dkt. Ben Rugangaza, akizungumza na wageni waalikwa pamoja na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma mpya ya kwanza duniani ya kutuma na kupokea fedha kupitia Tigo pesa kati ya nchi mbili Rwanda na Tanzania leo jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
Tigo, imeanzisha huduma ya kwanza ya kipekee ya kutuma na kupokea pesa baina ya nchi mbili tofauti ambazo ni Tanzania na Rwanda.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Tanzania, Diego Gutierrez amesema aina hii ya huduma ni ya kwanza duniani kwa kuwa na uwezo wa kubadilisha fedha za kigeni kutoka kwa mtumaji hadi kwa mpokeaji.
Amesema kuwa huduma hiyo inatoa fursa kwa watumiaji wa Tigo nchini kutuma pesa kwa njia ya simu kwa kutumia huda ya Tigo pesa kwenda kwa watumiaji wa Tigo nchini Rwanda, na kinyume chake.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Tigo, huduma hiyo inamwezesha mteja kubadilisha fedha za kigeni moja kwa moja kwa shilingi za kitanzania au francs za Rwanda zinaweza zikabadilishwa kuwa fedha za nchi zinakopokelewa.
Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Tanzania, Diego Gutierrez akizungumza wakati uzinduzi rasmi wa huduma mpya ya Tigo pesa kati ya wateja wa nchini mbili Tanzania na Rwanda.
Gutierrez alisisitiza kuwa fedha ikishapokelewa kwenye simu, mteja anaweza kuitumia kulipia huduma zote zinazopatikana kwenye Tigo pesa au Tigo cash iliyopo Rwanda.
“Huduma hii mpya itaokoa muda mwingi wa wateja pamoja na fedha zao. Watumaji wa fedha za kimataifa wamekuwa wakienda sehemu za kubadilishia fedha za kigeni kuweza kubadilisha francs za Rwanda kuwa dola kasha kutuma hizo doal kupitia kwa mawakala wengien wa fedha,”
“Tunafurahi kuwapa wateja wetu nyenzo za kufanya miamala kwa wana Afrika mashariki wenzao. Tunashukuru kwamba kutokana na teknolojia yetu ya kisasa, wananchi wa Rwanda wanaweza kutuma pesa kwa familia, marafiki, pamoja na wafanyabiashara wenzao walioko nchini kwao,” amesema Gutierrez.
Mgeni rasmi Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Dkt. Ben Rugangaza na Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Tanzania, Diego Gutierrez wakiwasiliana kupitia "Video Conference" na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Bw. Francis Mwaipaja pamoja na Waziri wa Fedha nchini Rwanda Mh. Claver Gatete wakati wa kuzindua huduma hiyo mpya ya kwanza duniani ya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu kimataifa baina ya Rwanda na Tanzania na yenye uwezo wa kubadili fedha za kigeni.
Kwa upande wake, Tongai Maramba, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Rwanda, amesema “Tumefurahi kuanza kuwapa wateja wetu wa Tigo cash uwezo wa kutuma fedha kimataifa kupitia simu zao. Pia ni jambo zuri zaidi kwamba wateja wetu wamerahisishiwa kwa kuweza kupokea moja kwa moja francs za Rwanda kwa sababu kampuni nyingi za kutuma na kupokea fedha huwa wanatumia dola. Huduma hii haimpi wasi wasi wowote mteja kuanza kutafuta sehemu ya kubadilishia fedha,” amesema
Kwa upande Balozi wa Rwanda nchini, Mh. Dr Ben Rugangaza amesema kuwa mahusiano ya Rwanda na Tanzania yameanza muda mrefu kupitia njia za reli ya kati na barabara (Central Corridor) na sasa nchi hizi mbili zimepiga hatua kwenye maswala ya mawasiliano hasa katika mitandao ya fedha kwa njia ya simu za mkononi.
Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Tanzania, Diego Gutierrez akionyesha ujumbe mfupi mara baada ya Balozi wa Rwanda nchini Tanzania kumtumia pesa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda wakati wa kuzindua huduma hiyo mpya ya kwanza duniani.
Amesema lakini hivi sasa nchi hizi mbili sasa zinazungumzia swala la Tigo pesa na katika kuzindua moja ya huduma adhimu duniani ya kutuma na kupokea fedha na kubadilishana fedha kwa njia ya mtandao ni hatua muhimu katika historia ya nchi hizi mbili Rwanda na Tanzania.
Aliongeza pia kwamba takwimu zinaonyesha kwamba katika kufanya biashara Rwanda ilikuwa nchi ya saba duniani kufanya biashara kubwa na Tanzania na biashara zote kwa ujumla ilikuwa asilimia nne.
Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Bw. Francis Mwaipaja pamoja na Waziri wa Fedha nchini Rwanda Mh. Claver Gatete wakionekana kwenye "video conference" kutoka nchini Rwanda.
Mgeni rasmi Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Dakta Ben Rugangaza akiushukuru Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda mara baada ya uzinduzi huo kufanyika kupitia "Video Conference".
Baadhi ya wageni waalikwa, wafanyabiashara, wanahabari na baadhi ya raia wa Rwanda wakifuatilia tukio hilo la kihistoria kati ya Rwanda na Tanzania.
Baadhi ya wafanyakazi wa Tigo Tanzania waliohakikisha zoezi la Video Conference baina ya Tanzania na Rwanda limekwenda vizuri wakati wa uzinduzi wa huduma ya kwanza duniani ya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu Kimataifa.