Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania, Bw.Matina Nkurlu (katikati) akishuhudiwa na Msimamizi wa bodi ya Michezo ya kubahatisha nchini,Bw.Humudi Abdulhussein(kushoto)wakati akimpigia mshindi wa droo kubwa ya mwezi ya promosheni ya Timka na Bodaboda Bi. Jovita Mosha(44)mkazi wa Ubungo external jijini Dar es Salaam aliyeibuka na kitita cha shilingi Milioni 30.kulia ni Mkuu wa kitengo cha Mtandao na huduma za ziada wa kampuni hiyo Bw.Charles Matondane.
Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania,Bw.Matina Nkurlu,akisisitiza jambo kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani)kuhusiana napromosheni hiyo ilivyobadilisha maisha ya wateja wao na watanzania kwa ujumla,mara baada ya kumtangaza mshindi wa droo kubwa ya mwezi ya"promosheni ya Timka na Bodaboda" Bi.Jovita Mosha(44)mkazi wa Ubungo external jijini Dar es Salaam aliyeibuka na kitita cha shilingi Milioni 30.
---
Ilikuwa ni safari ndefu na yenye mafanikio kwa wateja wa Vodacom Tanzania walioshiriki promosheni ya timka na boda boda kwani wengi wao wamefanikiwa kujishindia piki piki ambazo zimekuwa ni mkombozi mkubwa katika usafiri na kama njia ya kipato huku fedha taslimu zikiwainua vilivyo wajasiriamali ambao mtaji ulikuwa ni kilio chao kikubwa.
Promosheni hiyo leo imefikia tamati wakati wa droo iliyochezeshwa makao makuu ya kampuni hiyo ambapo Bi Jovita Leoni Mosha (44) ambaye ni Mkazi wa Ubungo External, ameshindia kitita cha shilingi Milioni 30 katika droo hiyo kubwa ya mwezi.
Akizungumza kwa njia ya simu mshindi huyo Bi. Mosha, amesema kuwa ni kama ndoto kwake kujishindia kiasi hicho kikubwa cha fedha lakini ndio kweli imetokea hususani mwanzo wa mwaka ambapo fedha imekuwa ngumu kwelikweli ukizingatia karo za shule, nyumba na mambo mengine lazima yalipwe.
"Nina furaha sana kuwa mshindi wa timka na boda boda,nilikuwa nategemea kushinda siku moja lakini si kiasi kikubwa kama hiki. Fedha hizi zitanisaidia sana katika shughuli zangu za kibiashara na familia kiujumla. Natamani kama promosheni ndio ingekuwa inaanza." Alisema.
Bi Mosha, Aliongezea kuwa kwa kipindi kirefu sasa alikuwa anakabiliwa na changamoto ya kupata mtaji katika shughuli zake za Ujasiriamali wa kuuza sabuni za maji. "siku zote nlikuwa nikiumia moyo kuona wenzake wakishinda kwani naye alikuwa akituma na kujibu maswali kila siku, lakini Mungu ni Mwema leo bahati imekuwa kwangu".
"Nachoweza kusema ni kwamba promosheni hii imekuwa mkombozi wa maisha ya washiriki na washindi wengi kwani washindi wengi wamekuwa wakionesha kuwa na malengo mazuri ya namna gani watakavyotumia zawadi zao iwe ni boda boda au fedha taslimu." Alisema Bi. Mosha na kumalizia "Nawasihi Vodacom waje na promosheni mpya ambayo tutanufaika nayo kama hii ya kihistoria kwangu ya timka na bodaboda."
Naye kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu akizungumza wakati wa droo hiyo alisema kuwa ana furaha sana kuona promosheni hiyo imekwisha kwa mafanikio makubwa ya kuweza kubadilisha maisha ya watanzania zaidi ya 700.
"Leo tunahitimisha promosheni ya timka na boda boda kwa kumpata mshindi wetu wa fedha taslimu kiasi cha shilingi Milioni 30 kupitia droo kubwa ya mwezi." Alisema Nkurlu,na kuongeza "mbali na mshindi huyu pia kuna washindi wengine watano wamejishindia boda boda."
Aliendelea kwa kusema kuwa mpaka zoezi hili linakamilika tayari tumekwishashuhudia boda boda 430 na fedha taslimu jumla ya milioni 330 zikikabidhiwa kwa washindi mbali mbali kutoka sehemu tofauti tofauti nchini.
"Washindi wa fedha taslimu wamethibitisha kuwa ulikuwa ni muda muafaka kwao kuongezea mitaji yao na biashara kukua na pia kwa wale ambao walikuwa na ndoto ya kufanya biashara sasa wamekamilisha malengo yao."
"Mfano mzuri ni dada Haika wa Arusha ambaye alijishindia Milioni 10, alikuwa ni mfanyashara wa duka tu lakini kwa ushindi ule aliahidi kuboresha zaidi biashara yake.
Naye Bw. Urio ambaye ni fundi viyoyozi, yeye alijishindia shilingi milioni 20 ambapo kitu kikubwa alichodhamiria kukifanya ni kujiendeleza kimasomo kwani yeye ni fundi makenika na anaamini akijiendeleza kimasomo litakuwa ni jambo zuri sana kwake." Alihitimisha Nkurlu.