MTIBWA Sugar imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa kirafiki kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa leo.
Simba walikuwa wa kwanza kubisha hodi kwenye lango la Mtibwa Sugar kwenye dakika ya 12 lakini shuti la mshambuliaji mpya wa timu hiyo Ally Badru liliishia mikononi mwa kipa Hussein Sharif. Kabla ya kupiga shuti hilio dhaifu Badru alikuwa amepata pasi ya Said Ndemla.
Mtibwa Sugar walijibu mapigo kwenye dakika ya 25 lakini mshambuliaji wake Jamal Mnyate alikosa bao la wazi kwa shuti alilopiga kutoka pembeni kidogo ya lango la Simba.
Timu hiyo kutoka mkoani Morogoro ilitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza nusura wapate bao kwenye dakika ya 27 lakini beki wa Simba Gilbert Kaze aliokoa mpira uliokuwa unatinga wavuni wa mshambuliaji Masoud Ally.
Simba walifanya shambulizi la kushtukiza lakini mshambuliaji wake Betram Mwombeki alipoteza nafasi nzuri ya kufunga kwenye dakika ya 33 akiwa peke yake na goli lakini shuti lake lilitoka pembeni kidogo ya lango la Mtibwa Sugar.
Dk 65 Ally Masoud aliifungia Mtibwa Sugar bao la kuongoza baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Hussein Ramadhani.