MHESHIMIWA Rais wangu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Nakusalimu kwa salamu ya utii inayotambua na kuheshimu kwa dhati mamlaka makubwa na ya juu uliyonayo kama mkuu wa taifa letu ambalo mazingira yake ya leo yanapaswa yawe wenye mwelekeo wa kushangilia kama si kujivunia uhuru ambao tuliupata mwaka 1961 na 1964 kwa kutegemea upande tulipo katika muungano wetu.
Mheshimiwa Rais, najisikia faraja iliyojaa majonzi moyoni kupata fursa hii adhimu kukuandikia waraka ambao msukumo wake unasukwasukwa na dhamira njema kabisa ambayo aghalabu kiini chake si kingine bali mapenzi mema kwa nchi na viongozi wetu wote.
Ni faraja kwa kuwa nimepata fursa ghali na adimu ya kuteta na kiongozi wetu mkuu kwa upendo, uhuru na kwa kujiamini, huku nikiwa na uchungu pia kwa sababu ujumbe ambao unabebwa na waraka huu ni wa kuumiza sana nafsi, roho, akili na mwili.
Mheshimiwa Rais, wewe ni kiongozi wa Watanzania wote tukiwamo sisi ambao baadhi ya wateule wako wameamua kwa sababu wanazozijua wao na wakati mwingine wakidai kwa maelekezo ya wakuu wao kutujengea taswira zinazotufanya tuonekane tu watu wa ovyo na kada ya wanajamii waliokosa utu na eti tunaopaswa kufundishwa hekima na somo la uzalendo ambalo limekuwa sehemu ya makuzi yetu nyumbani, shuleni, jeshini na ndani ya jamii.
Kabla sijafikisha ujumbe ambao nimeubeba kwa mfano wa mzigo mzito moyoni, napenda kwanza kupitia fursa hii kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na neema kwa kuniwezesha kuuona mwanga wa siku hii njema ya leo ambayo kama si kwa kudra na mapenzi yake, yumkini ingeongeza hesabu za siku ambazo kiwiliwili changu kingekuwa katika kaburi la sahau ambalo kila kukicha linameza roho za makumi kama si mamia ya Watanzania wasio na hatia wanaopoteza maisha kutokana na kazi za mikono ya majahili, miungu watu waliojitwalia haki ya kuchagua aina ya maisha na vifo vya watu wengine.
Baada ya hilo, kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania wenzangu ambao hawana fursa ya kuwasiliana nawe kwa njia kama hii ya waraka niliyoitumia, napenda kutumia pia wasaa huu kukushukuru wewe binafsi kwa namna ulivyojitoa usiku na mchana pasipo kuchoka kuliongoza taifa hili katika mazingira magumu yaliyojaa changamoto za kila namna ambazo wakati mwingine sina shaka hata kidogo kwamba zimekuwa zikikunyima raha na kukosa usingizi.
Wakati nikikuandikia ujumbe huu, picha na taswira yako inayonijia ni ile ya Machi 8, mwaka huu siku uliponitembelea kando ya kitanda nilichokuwa nimelazwa katika Hospitali ya Milpark, Johanesburg kule Afrika Kusini ikiwa ni siku mbili tangu nilipovamiwa, nikajeruhiwa na kupewa ulemavu na majahili ambao hadi leo hii wameweza kuukwepa mkono mrefu wa vyombo vya dola unavyoviongoza.
Mheshimiwa Rais, japo nilikuwa nina maumivu makali na machungu ya kupoteza jicho, kidole na kupasuliwa kwa mifupa ipatayo minane katika paji langu la uso, ukiacha taya lililoachanishwa kikatili na watesi wangu wale, bado ninaweza kukumbuka kwa ufasaha namna ulivyozungumza nami ukionyesha jinsi ulivyokuwa ukiguswa na kuumizwa sana na tukio lile.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, tangu niliporejea nchini miezi sita iliyopita sijapata kukutana nawe ana kwa ana ingawa nilipata fursa ya kukutumia salamu zangu za shukrani kupitia kwa marafiki zako kadhaa akiwamo msaidizi na mshauri wako nambari moja, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal ambaye siku zote wakati nikiwa katika matibabu nchini Afrika Kusini na hata baada ya kurejea nchini, alionekana kuwa mtu wa kukosa amani kabisa pasipo kunijulia hali kwa njia ama ya simu, wasaidizi wake na mwisho kwa kuonana nami ana kwa ana.
Nayarejea haya yote huku nikitambua kwamba, wakati ninapoandika waraka huu ndiyo kwanza umerejea kutoka nchini Marekani ambako ulikwenda kuchunguzwa afya yako ambayo nina matumaini makubwa ni njema hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa, ulikwenda huko siku chache tu baada ya kuiwakilisha vyema nchi yetu katika msiba mzito wa shujaa wa mapambano ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, mzee wetu, Nelson Mandela.
Ninapoyatafakari matibabu ghali niliyopata nchini Afrika Kusini kwa msaada wa mwajiri wangu na safari yako nchini Marekani, vinanikumbusha swali la mmoja wa wasaidizi wangu hapa ofisini aliyetaka kujua ni sababu gani hasa ambazo zimekuwa zikisababisha wasomi na viongozi wetu kuchunguzwa na kutibiwa katika hospitali za nje, tofauti na ilivyokuwa kwa Madiba ambaye kwa nyakati zote tangu afya yake ianze kumtatiza alikuwa akipata matibabu huko huko kwao Afrika Kusini?
Niseme kweli, japo nilikuwa na jibu au majibu ya swali lake, sikuwa na maelezo ya kutosheleza yaliyokuwa na mwelekeo wa kukata kiu ya swali lake, ingawa kwa kupapasa nilifanya kila juhudi kuutetea utaifa wangu na viongozi wake ilhali miye mwenyewe nikiendelea kukosa raha kwa namna nilivyokuwa nikitoa majibu ambayo yalikuwa yakionyesha hali ya kuukubali unyonge, kukiri ufukara, kuficha udhaifu wetu kama taifa na kutetea makosa ambayo aghalab ninyi viongozi wetu na wale wa kabla yenu mngeweza kuwa watu mliostahili kuwa na majibu halisi.
Rais wangu, swali na majibu vilisababisha kimoyomoyo, nijiulize maswali mengi mengine na moja ya maswali hayo yakiwa ni wapi tulipopotea njia hata tukafikia hatua ya kusababisha kuwa na kundi kubwa la watu waliokata tamaa, wanaoteswa na ufukara, ukosefu wa ajira na kila aina ya kero na karaha zinazozonga maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Rais, hali hiyo ilinipeleka moja kwa moja nchini Afrika Kusini na hususan katika Hospitali ya Milpark ambako huko ndiko miye mwenyewe na Watanzania wenzangu wengine tulikonusuru maisha yetu, huku baadhi kama ilivyo kwa Dk. Sengondo Mvungi wakipoteza maisha yao baada ya kukimbizwa huko.
Mheshimiwa Rais, naomba unisamehe kwa kulisema hili nitakaloliandika hapa kwamba, jibu nililolipata haraka haraka kuwa moja ya chagizo la matukio ya namna hii kutokea, halikuwa jingine bali ni kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa viongozi wetu hususan wale tuliowapa dhamana ya kuongoza sekta kadhaa nyeti kama ya afya na ustawi wa jamii.
Ushahidi wa kupwaya huko kwa viongozi hususan wale walio chini yako, ndiko huko huko ambako kumedhihirika pia wiki iliyopita bungeni Dodoma, ambako tulishuhudia zahama nyingine iliyowang’oa madarakani mawaziri wako muhimu wanne kwa sababu kama hizo hizo za mkwamo wao au watendaji wa chini yao katika kusimamia ipasavyo na kuchukua hatua kwa wakati, kila yatokeapo matatizo yanayogusa maeneo wanayoyaongoza.
Nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu, mheshimiwa Rais iwapo nitaficha shauku ya moyo wangu ambayo ilikwenda sambamba na tukio lile la Dodoma lililowagusa baadhi ya mawaziri ambao anguko lao linaweza likaelezwa kuwa ni ‘ajali ya kisiasa’ nikitumia msamiati ulioutumia wewe mwenyewe kwa mara ya kwanza ulipozungumzia tukio la kujiuzulu kwa waziri wako mkuu wa kwanza, Edward Lowassa.
Haja ya moyo wangu, nikiwa mhariri, mwanahabari, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na mdadisi wa kawaida tu wa mambo, ilikuwa kuona anguko la namna hiyo hiyo likimfika Waziri wa Habari ambaye amethibitisha pasipo na shaka kuwa pamoja na kuwa msomi wa Shahada ya Falsafa (Phd), ni kiongozi asiyejua anachofanya kwa kiwango cha kuwa mtu ambaye vichwa vya watu wengine ndivyo vinavyofikiri kwa niaba yake.
Nilitamani afikwe na zahama hiyo si kwa sababu ya kuwa na hasira au kumchuria mabaya, bali kwa kuzingatia ukweli kwamba yeye ni mtu ambaye bado anasongwa na matongotongo ya mfumo wa kibabe wa zama za magazeti ya Serikali na yale ya chama tawala, ambayo yanalazimika kuandika yale tu yanayofurahisha nyoyo na akili za watawala.
Mheshimiwa Rais, ingawa natambua na kuheshimu ukweli mchungu kwamba, suala la nani awe waziri na nani asiwe ni jambo la wewe mwenyewe kupenda na kuchagua na kwamba ulishasema mapema kabisa mbele yetu kwamba urais wako hauna ubia, bado naamini pia kwamba, wewe ni mtu msikivu na mkweli uliye tayari kusikia na kustahimili mambo mengi machungu unayokabiliana nayo kila siku.
Kwa sababu hiyo, basi napenda kukueleza kwa kuweka kumbukumbu sahihi ili mbele ya safari kabla na baada ya kumaliza urais wako uje kuyatafakari na kuukumbuka ushauri huu kwako kwamba, waziri uliyempa dhamana ya kulea na kuendeleza vyombo vya habari, ni mtu wa kuhofiwa, jeuri, mwenye kiburi, asiyeshaurika na dikteta asiyekutakia mema wewe binafsi, vyombo vya habari, serikali yako na taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa rais sijui kama unajua kwamba tangu umteue amefanya kazi na vyombo vya habari vya umma na hata baada ya sisi kufanya juhudi kubwa ya kuwa karibu naye kikazi kwa makusudi na kwa ujeuri mkubwa, amekataa wito na kupuuza maoni na ushauri wetu na kwa namna ya kusikitisha amesikika akitamba waziwazi kwamba anao uwezo wa kulifungia au kulifutia usajili gazeti lolote ambalo ataliona linakwenda kinyume cha maadili ya uandishi wa habari.
Waziri huyu ambaye alitarajiwa kuwa na silika za kuwa mlezi bora kutokana na jinsia yake na historia yake ya kupata kuwa mwanaharakati kabla ya kuingia serikalini, ndiye ambaye mamlaka makubwa uliyomtwisha, ameyageuza na kuwa mwavuli wa kuvisulubisha vyombo vya habari vyenye uthubutu wa kukosoa serikali na kuandika ukweli mchungu ambao asingependa kuona ukiripotiwa.
Mheshimiwa Rais, pengine baya zaidi kwa tasnia hii ni kwamba waziri huyo ana bahati mbaya ya kuwa na mmoja wa wasaidizi na washauri wake katika sekta yetu ya habari ambaye naye, hulka zake tangu aingie katika tasnia ya habari amekuwa ni mtu wa kujipendekeza, kupenda makuu, kuzusha na kutokuwa na mawazo huru. Huyu si mwingine bali Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO).
Ni jambo la bahati mbaya kwamba waziri huyu msomi pengine kwa sababu ya kutojua vyema rekodi na historia ya msaidizi wake huyo, ambaye japokuwa naye pia ni mteule wako, amejikuta akiwa mhanga wa fikra pandikizi zinazopenyezwa wizarani chini ya uratibu mahususi unaofanywa na baadhi ya wateule wako ambao wameshaanza kujipanga kusaka urais baada ya wewe kustaafu.
Mheshimiwa Rais, nimelazimika kuyasema yote haya baada ya kula kiapo cha moyoni huku nikirejea mafunzo tuliyokuwa tukikaririshwa utotoni chini ya imani ya wana TANU, ambayo hata sisi ambao hatukuwa wanachama wa chama hicho tulilazimika kuikariri kwa kuitamka kila kukicha; ‘Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.’
Rais wangu, gazeti la MTANZANIA limerejea tena mitaani. Japokuwa ni rahisi kuhesabu miezi, napenda kukueleza kwamba, ilikuwa ni miezi mitatu michungu sana kwetu kihisia na katika hali halisi.
Nitakuwa mzushi sawa sawa na hao ninaowashangaa leo, iwapo nitasema kulikuwa hakuna hitilafu au makosa ya kiuandishi ambayo yaliwapa kisingizio cha mikakati waliyoipanga mapema kabisa, wasaidizi wako hao kwa kulifungia gazeti letu hili.
Mheshimiwa Rais, nasema haya kwa sababu ni ukweli ulio bayana kabisa kwamba, habari zilizoandikwa na kutoa mwanya kwa serikali yako kutuadhibu gazeti hili, hazikulenga kuchochea na wala hazikuchochea kabisa chuki yoyote dhidi ya yeyote na mamlaka unazoziongoza kwa namna na kwa njia yoyote ile.
Siyo siri hata kidogo, mkurugenzi aliyetangaza uamuzi huo alifanya hivyo akijua watu wengi hawajui mapito na dhamira yake. Tunajua yeye alimshauri vibaya waziri na serikali huku akijua vyema kwamba, yuko hapo alipo kwa maelekezo mahususi ya kundi la watu wenye malengo binafsi ambao mheshimiwa rais, niko tayari wakati wowote na mahali popote kukueleza kwa kina na kwa undani ili wakati utakapotaka kuchukua maamuzi ya haki na kweli ujue undani halisi wa mambo haya.
Leo hii wakati tukirejea tena sokoni, tayari tumeshasikia kuendelea kuwapo kwa mikakati ile ile ya kuhakikisha gazeti hili na jingine ambalo halipendwi na watu hao hao kwa sababu binafsi yakiinaingizwa tena mtegoni na kufungiwa kifungo kingine kama hiki tulichomaliza au kinachofanana na kile kilichoifika MwanaHalisi.
Mheshimiwa Rais, naandika waraka huu nikikumbuka semi zako mbili unazotumia; ‘tunajenga nyumba moja kwanini tugombee fito?’ na ile ya ‘akili za kuambiwa changanya na zako’ ambazo kwa muktadha wa waraka wangu huu kwako zinaweza zikawa za msaada sana kwako na pengine kwetu sisi wa MTANZANIA ambao tunashangilia kurejea mtaani kwa gazeti letu lililodhulumiwa fursa ya kuchapwa kwa muda wa siku 90.
Nimelazimika kukutumia wewe Rais si kwa lengo la kuchosha akili zako au kukupotezea muda, isipokuwa kwa kutambua hadhi, heshima na mamlaka makubwa uliyonayo juu ya wateule wako hao ambao wameamua kwa sababu ya jeuri za kimamlaka walizonazo kuumiza watu na kutupa sifa na majina mabaya tusiyostahili. Hakika wazungu walikuwa sahihi waliposema ‘power currupts’.
Mheshimiwa Rais, lingekuwa ni jambo la kheri kwa Serikali na kwa taifa letu zima iwapo kusudi la kufungia magazeti linalopangwa na wateule wako kuwa utamaduni wa kudumu, lingekuwa ni kujenga mustakabali mwema kwako wewe binafsi, chama chako, Serikali unayoiongoza na nchi yetu kuliko hili la sasa lenye dhamira ya kufunga watu midomo, kutesa, kuzusha na kuharibu taswira yetu kama watu binafsi, taasisi na taifa.
Ni kwa sababu hizo, mheshimiwa Rais ndiyo maana baada ya kusukwasukwa na moyo na kuumizwa mno kifikra nikaona nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu na haki za maelfu ya Watanzania ambao tunaamini wanahitaji huduma ya magazeti haya katika kukidhi mahitaji yao muhimu ya kimaisha, kielimu na kiufahamu kila kukicha na kuacha dhamira hizi za kishetani zikiendelea kuongoza sekta yetu.
Mheshimiwa Rais, siyo siri hata kidogo kwamba, ingawa mawazo hasi dhidi ya uhuru wa kikazi na kiwajibikaji wa vyombo vya habari na wanahabari yanaonekana kutawala kauli na maamuzi ya baadhi ya viongozi na washauri wako kwa kiwango cha kukushawishi hata wewe binafsi kukubaliana nayo, ukweli ni kwamba, nyuma ya maneno matamu wanayotumia kutupaka matope, kutujeruhi na kutupa kila aina ya sifa mbaya kuna ajenda za kutuharibia sisi, kukuharibia wewe, kukomoa, kuumiza na zaidi kulikwamisha taifa.
Nitakuwa mhariri nisiyewajibika, iwapo nitakaa kimya ilhali nikijua fika kwamba, leo hii ndani ya wizara iliyopewa dhamana ya kulea vyombo vya habari, baadhi ya wateule wako na watendaji wake wamekalia viti walivyonavyo si kwa sababu ya kuwa kwao na uwezo kustahimili ukosoaji, au upeo wao wa kuchochea maendeleo ya kitaaluma, bali kwa kuendeleza na kuyatumikia matakwa ya utarishi wa kifikra na kimatendo.
Kwa waraka huu mheshimiwa Rais, wakati tukikuahidi kwa dhati kabisa wewe binafsi na Watanzania wenzetu kwamba, tutaendelea na kazi kwa kuzingatia miiko na maadili ya uandishi wa habari, sambamba na kuheshimu sheria zilizopo, tunapenda kuliweka hili bayana kwamba, tutakuwa wa mwisho kuwatii viongozi dhalimu, madikteta, waliokosa utu na ambao kwao hila ndiyo msingi mama wa kupotosha na kupindisha mambo kwa sababu tu ya kulinda maslahi na malengo yao binafsi au yale ya makundi yenye hila.
Rais wangu, nimeona nitakuwa mtu nisiyekutakia mema wewe binafsi na taifa kwa ujumla, iwapo nitakaa kimya na kuruhusu fikra za kikaburu zikijijenga vichwani mwa viongozi wetu.
Mheshimiwa Rais, tutakuwa tumeshindwa kutimiza wajibu wetu kama wanahabari, wahariri na viongozi iwapo tutahalalisha kwa sababu ya ukimya wetu majina mabaya tunayoitwa leo na wateule wako kama wasaliti, wachochezi na wazushi.
Miye binafsi naamini kwa dhati kabisa kwamba iwapo wewe utaamua kwa moyo na nia njema kulinusuru taifa letu na majahili hao walio ndani ya Serikali yako, basi siku moja historia itakuja kuandika kwa usahihi na ufasaha jina lako na letu..
Mungu ibariki Tanzania.