JESHI la Polisi, limekuwa la kwanza kati ya taasisi saba zinazohusika moja kwa moja, kukiri udhaifu katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyowaondoa mawaziri wanne katika nafasi zao.
Mawaziri ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais Jakaya Kikwete Ijumaa iliyopita kutokana na kadhia hiyo kwa Taifa, ni Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mungulu, alisema yaliyojiri katika Operesheni hiyo, ni moja ya changamoto kubwa zilizowasibu kwa mwaka huu.
“Operesheni Tokomeza Ujangili, ni moja ya changamato ambazo zimetusibu kwa mwaka huu. Kama kujisahihisha basi tutajisahihisha. “Yaliyotokea tumeyaona … operesheni hazitakiwi kuleta madhara makubwa na kama yanakuwapo basi yanapaswa kuwa kidogo,” alisema.
Alisema kwa kuwa mchakato wa kujirekebisha kutokana na makosa yaliyofanyika katika Operesheni hiyo unaendelea, wananchi watarajie mabadiliko.
“Kuhusu nini kifanyike pia ni suala la kufuatilia. Tunachukua taarifa kama ilivyotolewa na kwa vile mchakato unaendelea, nadhani tutaona mabadiliko zaidi,” alisema Mungulu.
Mungulu ametoa kauli hiyo wakati Rais Kikwete akisubiriwa na umma wa Watanzania, kuchukua hatua ya kujaza nafasi hizo, ambazo zinatarajiwa huenda zikahusu mabadiliko zaidi katika wizara zaidi ya hizo nne huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akitangaza hatua zaidi zitakazofuata.
Katika hatua hizo, Pinda alisema itaundwa Tume ya Uchunguzi wa Kimahakama, ambayo Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema alisema ndiyo itakayomaliza mzizi wa fitina.
Taasisi nyingine.
Tume hiyo inatarajiwa katika uchunguzi wake, kufikia Jeshi la Polisi lililokuwa na askari 440 katika Operesheni hiyo.
Taasisi zingine zinazotarajiwa kufikiwa na Tume hiyo, ambayo Rais Kikwete ameagiza uundwaji wake uharakishwe, ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambalo lilikuwa na askari 885 katika Operesheni hiyo.
Zingine kwa mujibu wa ripoti hiyo ya James Lembeli, ni Kikosi Dhidi ya Ujangili askari 440, Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), lililokuwa na askari wa wanyama pori 383.
Pia kuna Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), iliyokuwa na askari 99, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), iliyokuwa na askari 51, Wizara ya Sheria na Katiba iliyokuwa na waendesha mashitaka 23 na Idara ya Mahakama iliyokuwa na mahakimu 100.
Mbali na taasisi hizo, tayari jana kulitolewa kauli za viongozi na mashirika mbalimbali yakitaka watendaji zaidi katika wizara husika, wachukuliwe hatua baada ya viongozi wao kuwajibika kisiasa.
Haki za binadamu.
Ripoti hiyo ya Operesheni Tokomeza Ujangili imeainisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kuwahi kutokea katika historia ya nchi.
Mbali na kutokea mauaji ya watumishi sita na watuhumiwa 13, ripoti hiyo ilibainisha udhalilishaji na mateso kwa binadamu yaliyofanyika.
Miongoni mwa mateso hayo, ripoti hiyo ilibainisha kuwa viongozi wa vijiji na vitongoji na watumishi wa Serikali walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza.
“Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa, walidai walidhalilishwa mbele ya wanafamilia kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu zao za siri bila ridhaa yao.“Ndugu Ali Nyenge (38) wa Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga, alidai kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji yaliyochanganywa na chumvi na kuchapwa viboko huku mwanawe wa kiume wa umri wa miaka 11 akishuhudia,” ilieleza taarifa hiyo.
Pia kwa mujibu wa taarifa hiyo, alidai kutakiwa kuchora picha ya chatu kwa kutumia wembe kwenye paja lake.
“Baadhi ya akinamama walidai kubakwa na kulawitiwa, mfano kata ya Iputi, wilaya ya Ulanga, mwanamke mmoja alidai kubakwa na askari wawili usiku. “Mama mmoja mkazi wa kata ya Matongo, wilayani Bariadi, alibakwa na askari watatu huku akiwa ameshikiliwa mtutu wa bunduki,” taarifa hiyo ilieleza.
Kwa viongozi, Diwani wa kata ya Sakasaka wilayani Meatu, Peter Samwel, alidai kuadhibiwa akiwa mtupu, kuning’inizwa kichwa chini miguu juu, kupigwa kwa nyuma na kulazimishwa kufanya mapenzi na mti.
“Baadhi ya kambi za mahojiano zilipewa jina kama vile Guantanamo (Ruaha), Goligota (Ngorongoro), Duma na Andajenga (Serengeti),” ilieleza ripoti hiyo.
Wizara nyingine kukumbwa ?.
Ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili, imewaondoa katika nafasi zao mawaziri hao wanne, huku kukiwa na vuguvugu la tuhuma za mawaziri wasiowajibika ipasavyo waliopewa jina la mawaziri ‘mizigo’ na chama chao cha CCM.
Vuguvugu hilo lilianzia katika ziara ya zaidi ya mwezi mmoja ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana mikoani ambapo inadaiwa wananchi walibainisha mawaziri wasiowajibika kuwa ni pamoja na Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika), na Naibu wake, Adam Malima.
Wengine walitajwa ni William Mgimwa (Fedha), Dk Shukuru Kawambwa (Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara).
Habari kwa hisani ya HABARILEO.