Na mwandishi Wetu, Dar
Jumla ya wanafunzi 100 wa fani za uuguzi na ukunga, wanatarajia kupata ufadhili wa masomo kutoka Shirika la Utafiti wa tiba na afya Barani Afrika (AMREF) kuanzia mwaka ujao wa masomo.
Ufadhili huo unatokana na makusanyo ya jumla ya shilingi Milioni 437 yaliyopatikana katika hafla maalum iliyoandaliwa na AMREF Oktoba mwaka huu, kuchangia fedha kwa ajili ya kuwasomesha wakunga, kwa lengo la kupunguza uhaba wa wahudumu hao wa sekta ya afya hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa AMREF Tanzania Dr Festus Ilako, alisema jana jijini Dar es salaam kuwa wanafunzi watakaopata ufadhili huo, watasaidia katika kupunguza vifo vya akinamama wajawazito ambavyo hutokea wakati wa kujifungua.
Dr Ilako alisema vifo vya wajawazito vimefikia wanawake 455 kwa kila wanawake laki moja, na hivyo Tanzania kuhitaji wakunga na wauguzi wengi zaidi ili kuweza kupunguza idadi ya vifo hivyo.
“Jukumu la kuokoa maisha ya mama wajawazito ni jukumu letu wana jamii na kwahiyo sisi AMREF tumeamua kutoa mfano huu kwa kusomesha wakunga 100 kuanzia mwaka ujao wa masomo na tunashukuru wahisani kadhaa waliokubali kutuunga mkono katika swala hili”, alisema Dr Ilako.
Aliongeza kuwa bado shirika lake linaendelea kupokea michango toka kwa wahisani nmbalimbali, ili lengo la kusomesha wakunga 3,800 ifikapo mwaka 2015 liweze kutimia na hivyo kusaidia kupunguza pengo la uhaba wa wakunga kaika hospitali mbalimbali nchini.
Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Benki M Bi Jacquiline Woisso, alisema taasisi yake imechangia shilingi Milioni 100 kwa AMREF ili kutimiza lengo lao la kusomesha wakunga wengi zaidi, na hivyo kusaidia jitihada za serikali kupata watalamu wengi zaidi katika sekta hiyo ya afya.
“Sisi Benki M tumeona kuwa kinachofanywa na AMREF ni jambo la msingi kwa ajili ya kuokoa maisha ya akinamama wajawazito ambao wengi hufariki wakati wa kujifungua. Na hii ndio imetupa sisi sababu ya kutoa mchango huu tukiamini watu wengine na mashirika binafsi yataiga mfano huu ili kusaidia maendeleo katika sekta ya afya hapa nchini”, alisema Bi Woisso.
AMREF kwa kushirikiana na wadau kadhaa, iliendesha hafla maalum Oktoba mwaka huu kuchangia mfuko wa kusomesha wakunga na wauguzi kwa lengo la kupunguza pengo la wataalamu hao katika hospitali mbalimbali nchini.
Zaidi ya shilingi Milioni 437 zilikusanywa katika hafla hiyo iliyoongozwa na Makamu wa Rais Dr Mohamed Ghalib Billal, ambapo lengo ni kukusanya fedha zitakazoweza kusomesha wakunga 3,800 ifikapo mwaka 2015.