WAZIRI wa Viwanda na Biashara ambaye pia ndio mbunge wa Handeni, Dkt Abdallah Kigoda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Utamaduni, lililopangwa kufanyika Katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni mkoani Tanga, Desemba 14 mwaka huu.
Tamasha hilo linafanyika kwa mara ya kwanza wilayani hapa, huku likitarajiwa kuwa la aina yake kutokana na maandalizi yanayoendelea kushika kasi, ambapo kwenye uwanja huo, Tamasha hilo litaanza saa 2 asubuhi hadi saa 12 za jioni.
Akizungumza jana mjini Handeni, Mratibu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema maandalizi yamezidi kushika kasi kwa kuangalia mazoezi ya vikundi kadhaa vitakavyotoa burudani katika tukio hilo.
“Tunashukuru Mungu kuona mambo yanazidi kuwa mazuri kwa kuhakikisha kuwa Desemba 14 mwaka huu tunafanya tamasha lenye mguso na kila mmoja wetu kufaidishwa.
“Huu ni wakati wa kila mtu kujipanga ili aje kushiriki kwa namna moja ama nyingine, ukizingatia kuwa juhudi hizi zote zipo kwa ajili ya kujenga ushirikiano kwa watu wote,” alisema Mbwana.
Wadhamini katika tamasha hilo ni pamoja na gazeti la Mwananchi, Clouds Media Group, ni Phed Trans, Clouds Media Group, Grace Products, Screen Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles & Construction Ltd, Katomu Solar Specialist, PLAN B SOLUTIONS (T) LTD, Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group duka la mavazi la Chichi Local Ware, Smart Mind & Arters chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog, Pamoja Pure Blog na Taifa Letu.com.