Naibu Waziri wa mambo ya ndani, Bw. Pereira Silima (wa kwanza kushoto)akizungumzia umuhimu wa kupambana na ajali za barabarani leo katika hafla fupi ya kumtangaza Athmani Hamisi (wa tatu kutoka kulia)kuwa balozi wa usalama barabarani iliyofanyika katika ukumbi wa habari maelezo jijini Dar es salaam. Kulia ni Meneja wa Airtel Money Asupya Nalingigwa akifuatiwa na Mjumbe wa baraza la taifa la usalama barabarani Bw. Yakubu Rajabu.
Naibu Waziri wa mambo ya ndani, Bw. Pereira Silima (katikati) akisisitiza jambo juu ya umuhimu wa kila mwananchi kutii sheria bila shuruti ili kuepusha ajali za barabarani wakati wa hafla fupi ya kumtangaza Athmani Hamisi (kulia)kuwa balozi wa usalama barabarani iliyofanyika katika ukumbi wa habari maelezo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi DCP Mohamed Mpinga.
Balozi wa kampeni ya nenda kwa usalama barabarani, Bw. Athmani Khamisi akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutangazwa rasmi kuwa balozi wa kampeni ya nenda kwa usalama barabarani iliyofanyika katika ukumbi wa jengo la habari maelezo jijini Dar es salaam hivi karibuni. Kulia kwake ni Mjumbe wa baraza la usalama barabarani Bw. Yakubu Rajabu.
---
Airtel, Baraza la Taifa la Usalama barabarani waungwa mkono na wananchi Baadhi ya wananchi wanaoishi jijini Dar es salaam wamesema uamuzi uliofikiwa na Baraza la Taifa la Usalama Barabarani wa kumtangaza aliyekuwa mpiga picha wa magazeti ya serikali Bw. Athmani Hamisi kuwa balozi wa kampeni ya usalama barabarani una maana kubwa sana.
Wananchi hao wameyasema hayo katika nyakati tofauti walipokuwa wakiojiwa na mwandishi wetu juu ya kampeni hii ya nenda kwa usalama barabarani inayodhaminiwa na Kampuni ya mitandao ya simu za mkononi ya Airtel.
Wananchi wengi wamesema uamuzi huo wa kumteua Bw. Hamisi kuwa Balozi wa kampeni hiyo kwa dhumuni la kutoa elimu ya usalama barabarani utakuwa na matunda zaidi kwa sababu kupitia yeye watu watajifunza vyema juu ya athari za ajali barabarani.
“Kumtumia mtu ambaye alishakuwa muhanga wa ajali ni jambo sahihi kabisa kwa sababu ataweza kutoa ushuhuda wa wazi ni jinsi gani ajali zimemkwamisha hata kwenye shughuli zake za kimaendeleo na kuwaasa vyema watu wanavyotakiwa kujikinga na ajali hizo.” Alisema Calisti Mushi mkazi wa Temeke jijini Dar es salaam.
Kwa upande mwingine baadhi ya wakazi wa sehemu mbalimbali za jiji la Dar es salaam walisema ni kweli kuwa jukumu la kupinga ajali ni la kila mwananchi lakini elimu zaidi inapaswa kutolewa ili kuzitokomeza kabisa.
“Bado elimu inahitajika zaidi kwa watumiaji wa vyombo vya moto ili kuepusha ajali ambazo hutokea kila siku, na kwa kutumia wahanga wa ajali kama Bw. Hamisi watu wataelewa vizuri zaidi ni jinsi gani ajali hudumaza maendeleo ya taifa kiujumla” walisema baadhi ya wananchi waishio katika jiji la Dar es salaam.
Kwa upande wake Balozi huyo mpya wa kampeni ya usalama barabarani, Bw. Hamisi alisema atajitaidi kwa hali na mali kutoa elimu na kuwaasa wananchi kuwa makini wanapokuwa njiani kwani ajali zinazotokea hukwamisha maendeleo kwa kiasi kikubwa.
“Mimi binafsi nimepumzika kwa muda mrefu kutokana na ajali niliyoipata, nataka nitumie fursa hii kama balozi kuiasa jamii na kutoa elimu juu ya madhara ya ajali na nini tufanye ili tuweze kuziepuka” alisema Hamisi.
Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando alisema Airtel haitoacha kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Baraza la taifa la usalama barabarani katika kuokoa maisha ya watanzania ambayo hupotea kutokana na ajali za barabarani.
“Tunatambua umuhimu wa kuepusha ajali za barabarani na ndio maana tunaiunga mkono kampeni hii ya nenda kwa usalama barabarani kwa dhumuni la kuepusha vifo na majeruhi ambavyo hupatikana mara nyingi kwa kutokuwa na elimu ya usalama barabarani,” alisema Mmbando.
Kampeni ya nenda kwa usalama barabarani ina dhumuni la kutoa elimu kwa wananchi juu ya sheria za barabarani na itafanywa katika mikoa mbalimbali nchini.