Mhamasishaji Jamii kutoka Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malria, Makono Andrea, katikati, akizungumza na washiriki wa Shindano la kuimba la Epiq Bongo Star Search kuhusiana na mapambano dhidi ya Malaria. Kulia kwake ni Winnes Lyaro, balozi wa Malaria wa Zantel.
Mtaalamu wa Huduma na Bidhaa wa Zantel, Bi Emmiliana Vakolavene akielezea huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni ya Zantel kwa washiriki wa shindano la Epiq Bongo Star Search. Kulia kwake ni Mkufunzi wa wataalamu wa Mauzo, Abdallah Sinani na kushoto kwake ni Meneja Kitengo Huduma za Ziada, Haji Yusuf.
----
Washiriki 6 bora waliobaki kwenye jumba la Epiq Bongo Star Search leo wametembelea ofisi za Zantel ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na kampuni hiyo, ambayo ndio wadhamini wa shindano hilo kubwa la kuimba nchini.
Wakiwa ofisini hapo, washiriki hao ambao walipata fursa ya kutembelea vitengo vyote vya Zantel na kuuliza maswali kwa wakuu wa vitengo hivyo.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki hao, mshiriki kutoka Mandela Nicholaus alisema lengo kubwa la ziara hiyo ni kujifunza namna kampuni ya Zantel inavyotoa huduma zake.
‘Tumekuja hapa kujifunza namna kampuni ya Zantel inavyofanya kazi lakini sambamba na hilo ni kutoa shukurani zetu za dhati kwa udhamini wa Zantel kwenye shindano hili ambao hakika umefanya shindano kuwa la kipekee sana’ alisema Mandela.
Washiriki hapo pia walipata fursa ya kujifunza kuhusiana na namna ya kupambana na ugonjwa wa Malaria.
Naye, Afsa Biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan akizungumza wakati wa kuwakaribisha washiriki hao kwenye ofisi za Zantel, aliwapongeza kwa kuja kuwatembelea na kujionea namna wanavyofanya kazi.
‘Kwanza niwapongeze kwa kufikia hatua hii ya sita bora kwani mmepita vikwazo vingi toka usaili ulipoanza, na sisi Zantel tunaahidi kuwa tutaendelea kuwaunga mkono hata baada ya mashindano haya kuisha’ alisema Khan.
Washiriki waliotembelea Zantel ni Melisa John ambae namba yake ya kupigiwa kura ni 22, Amina Chibaba (03), Emmanuel Msuya (21), Maina Thadei (15), Mandela Nicolaus (10) na Elizabeth Mwakijambile (08).
Shindano hilo ambalo sasa linafanya matamasha kwenye sehemu mbalimbali, ambapo wiki iliyopita lilikuwa Temeke-Mwembe Yanga, na jumapili hii litakuwa Mbagala viwanja vya Zakheem kuanzia saa nane mchana.
Kwa sasa, shindano la kuimba la Epiq BSS liko katika hatua za mwisho, huku fainali yake ikitarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Escape hapo tarehe 30 mwezi wa kumi na moja.