Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imefuatilia taarifa kwenye vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini, kuhusu kushiriki kwa Mheshimiwa Lu Younqing Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika huko Shinyanga, mwishoni mwa juma lililopita.
Taarifa hizo zimeambatana na picha zinazomuonyesha Mheshimiwa Lu akiwa amevaa kofia yenye nembo ya CCM. Habari zinaeleza kuwa Balozi alikwenda Shinyanga kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong, na viwanda hivyo vita kuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika mwakani.
Wizara inatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Jamhuri ya watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vilevile inatambua kazi nzuri ambayo Balozi Lu Younqing amekuwa akifanya toka alipowasili nchini Tanzania.
Kutokana na tukio hili, Wizara inapenda kuelekeza kwamba kitendo cha Balozi yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa sio sahihi na kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia. Mkataba huo wa Vienna unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi ikiwemo siasa wanapofanya kazi zao kwenye nchi za uwakilishi. Aidha, Sheria ya Diplomasia ya Tanzania ya Mwaka 1986 ambayo ni zao la Mkataba wa Vienna pia hairuhusu Balozi au mfanyakazi wa Ubalozi kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi.
Itakumbukwa kwamba, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012 Wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki. Na kwa tukio hili pia Wizara imechukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili lisitokee tena.
IMETOLEWA NA:
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
18 Septemba, 2013
Dar Es Salaam.