Mfungaji nyota wa timu ya Utumishi, Anna Msulwa akifunga goli huku mchezaji wa Taswa Queens, Elizabeth Mbassa akiwa hana la kufanya katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Leaders Club. Utumishi ilishinda kwa mabao 43-19
---
Na Mwandishi Wetu
BAADA ya kutamba kwa muda mrefu bila kufungwa, timu ya netiboli ya waandishi wa habari za michezo nchini (Taswa Quuens) juzi ilichezea kichapo kikali cha mabao 43-19 kutoka kwa timu ya Utumishi katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Leaders Club.
Taswa Queens ambao ni mabingwa wa Tamasha la Waandishi wa Habari la Arusha, haikuwi kufungwa tokea kuanzisha kwake mwezi Aprili mwaka huu.
Katika mchezo huo, Taswa Queens ilianza kwa kasi kupitia wafungaji wake, Zainabu Ramadhan na Imani Makongoro na kufunga 3-0 katika dakika za mwanzoni kabla ya Utumishi kutumia mfungaji wake nyota, Anna Msulwa (GA) kubadili kibao na kuanza kuisambaratisha Taswa Queens.
Msulwa ambaye alikuwa nyota wa mchezo, alionyesha uwezo mkubwa akishirikiana na GS wake, Fatuma Machenga na kuweza kuongoza kwa mabao 22-10 hadi mapumziko.
Taswa Queens iliweza kucheza vizuri pamoja na kichapo hicho na kutokuwepo kwa mchezaji wake, Sharifa Mustafa kulisababisha timu hiyo kutoweza kucheza vizuri.
Utumishi iliwatumia wachezaji wake nyota ambao wanatamba katika mchezo wa netiboli nchini kama Amina Ahmed ambaye pia anachezea Don Bosco kwa upande wa mpira wa kikapu, Elizabeth Fusi, Sharon Batenga, Monica Aloyce na Zaujia Abdallah.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Msulwa alisema kuwa mchezo huo ulikuwa wa maandalizi kwa ajili ya michezo ya Shimiwi na wamefarijika kuvunja mwiko wa Taswa Queens kwa kutofungwa.
“Taswa Queens ni timu nzuri na inaweza kufikia hatua kubwa zaidi kama itaweza kuongeza bidii, kwa Utumishi ni ishara tosha ya kufanya vyema katika michezo ya Shimiwi,” alisema Msulwa.