Na Veronica Kazimoto – Maelezo, Dar es salaam
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti, 2013 umepungua hadi kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 7.5 za mwezi Julai, 2013 kutokana na kupungua kwa bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Agosti 2013 leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo alisema kupungua kwa mfumuko wa Bei nchini kumechangiwa na kupungua kwa bei za Bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi kutoka asilimia 8.0 kwa mwezi Julai, 2013 hadi asilimia 6.5 za mwezi Agosti, 2013.
Kwesigabo alifafanua kuwa kasi ya ongezeko la bei kwa bidhaa zisizo za vyakula imebaki kuwa asilimia 7.3 kwa mwezi Agosti, 2013 kama ilivyokuwa mwezi Julai, 2013.
“Kupungua kwa Mfumuko wa Bei kunamaanisha kuwa, kuna unafuu wa maisha kwa mlaji; kwa maana hiyo Tanzania inaonyesha kuwa inapiga hatua nzuri katika uchumi wa nchi yetu”, amesema Kwesigabo.
Alizitaja bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kuwa ni pamoja na mikate na nafaka (asilimia 2.2), vitafunwa (asilimia 3.8), mahindi (asilimia 1.6), unga wa ngano (asilimia 2.5), unga wa muhogo (asilimia 0.6), mtama (asilimia 3.4) na kuku wa kienyeji (asilimia 0.9).
Bidhaa nyingine ni samaki wabichi (asilimia 2.6), karanga (asilimia 2.0), mbogamboga (asilimia 2.4), nyanya (asilimia 9.9), vitunguu maji (asilimia 2.0), viazi vitamu (asilimia 4.8), mihogo (asilimia 4.1) na sukari (asilimia 0.5).
Bidhaa zisizo za chakula zilizochangia kupungua kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na; viatu (asilimia 0.3), samani (asilimia 0.1), vyombo vya udongo (asilimia 1.0), na vifaa vya elekroniki vya kurekodia picha na sauti (asilimia 0.3).
Wakati huohuo Mkurugenzi Kwesigabo amesema kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania kwa mwezi agosti, 2013 imepanda ikilinganishwa na mwezi septemba 2010.
Akitolea mfano wa shilingi 100, Kwesigabo amefafanua kuwa uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umepungua hadi kufikia Shilingi 71 na Senti 46 kwa mwezi Agosti 2013.
“Hii inamaanisha kuwa, ili Mlaji aweze kununua bidhaa na huduma sawa na alizokuwa akinunua kwa Shillingi 100 mwezi Septemba, 2010 atahitaji Shilingi 28 na Senti 54 zaidi, yaani awe na Shilingi 128 na Senti 54 mwezi Agosti, 2013”, amesema Kwesigabo.
Mfumuko wa Bei nchini umeanza kuonyesha mwelekeo unaofanana na nchi jirani za Afrika mashariki hususani Kenya na Uganda.