Promota aliyeandaa pambano la Kimataifa la ubingwa wa dunia la uzito wa super middle kati ya bondia Francis Cheka na bondia kutoka Marekani, Phill Williams, Jay Msangi wa kampuni ya Hall of Fame Boxing and Promotion, anashikiliwa na Jeshi la Polisi katika Kituo cha Kati kwa tuhuma za kumdhulumu bondia kutoka Marekani.
Kamishna Msaidizi wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP Ahmed Msangi alisema jana kuwa promota huyo alikamatwa jana Jumamosi Mchana maeneo ya Oysterbay na kufikishwa kituoni hapo kwa mahojiano na uchunguzi zaidi.
ACP Msangi alisema kuwa promota huyo alihojiwa na Polisi kituoni hapo na kuendelea kumshikilia promota huyo hadi hapo uchunguzu wa suala hilo utakapokamilika.
Alisema mbali ya kumhoji promota huyo, pia waliweza kuchukua maelezo ya bondia Mmarekani Williams na meneja wake sambamba na Rais wa Organizesheni ya Masumbwi Tanzania (TPBO)- Limited, Yasin "Ustadh" Abdallah na wadau wengine waliohusika katika pambano hilo.
Aidha Msangi alifafanua kuwa bondia Williams anadai jumla ya Dola za Kimarekani 8,200,000 (sawa na shs Milioni 14) za Kitanzania kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa baina yao.
"Jambo linalodaiwa kufanywa na promota huyo ni aibu kubwa kwa Taifa, sisi tulikuwepo katika pambano hilo ambapo tulishuhudia baadhi ya mabondia wa Tanzania nao wakimalamikia huku wengine wakigoma kupanda ulingoni, kwa kutolipwa pesa zao, ni aibu kwa Taifa mbele ya wageni waliokuja kufanikisha pambano hilo ambalo Cheka alishinda kwa pointi," alisema Msangi.
Katika pambano hilo mwandishi wa habari hizi wa mtandao huu, aliwashuhudia baadhi ya mabondia kama Alphonce Mchumiatumbo, Thomas Mashali, Mada Maugo na Francis Cheka, wakigoma kupanda ulingoni kabla ya kulipwa pesa zao walizosainiana katika mkataba wao.
Hata hivyo, mabondia hao walipanda ulingoni baada ya kikao kilichoitishwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kilichofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee. Kikao hicho kiliamua kuwa promota Msangi kuweka rehani gari lake ambapo tayari mdau mmoja wa ngumi za kulipwa nchini alikuwa tayari kutoa Dola 12,000 za Kimarekani ili walipwe mabondia hao na wengine.
Promota Msangi alifanya ujanja na kutotoa gari lake, hali iliyopelekea kutokea matatizo makubwa ambayo yameiweka nchi katika aibu kubwa hasa katika mchezo wa ngumi.