Msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye amezidi kujijengea heshima ndani na nje ya nchi Nasib Abdul maarufu kama Diamond anatarajiwa kupagawisha wakazi wa mkoa wa Kigoma Jumamosi hii na style ya kipekee ya ‘Kikwetu Kwetu’ kwa hisani ya bia ya Kilimanjaro.
Msanii Diamond ataungana na wasanii wengine tisa wa muziki wa Bongo Fleva watakaotumbuiza katika tamasha la ‘Kili Music Tour 2013’ ambalo linatarajiwa kufanyika mjini Kigoma katika uwanja wa Lake Tanganyika siku ya Jumamosi.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager Bwana George Kavishe alisema kuwa “tamasha la Kili Music Tour linaelekea Kigoma baada ya kufanya vizuri jijini Mbeya, Mwanza, Dodoma, Tanga na Kilimanjaro. Wasanii kumi ambao watatumbuiza Jumamosi hii ni Diamond Plutnumz, Linex, Barnaba, AT, Fid Q, Prof J, Recho, Lady Jay Dee, Roma na Ben Paul.”
Bwana Kavishe aliendelea kufafanua kuwa amefurahishwa sana na jinsi watanzania wanavyopokea bonge la kiburudisho kutoka kwa bia yao ya Kilimanjaro. “ni faraja kubwa kuona jinsi style ya “kikwetukwetu” ilivyokubalika nchini kote. Kilimanjaro inaelewa fika kuwa watanzania wana mambo mengi sana ya kujivunia ambayo ni ya kipekee kikwetukwetu. Ukiachana na bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo inatengenezwa Tanzania, na watanzania, kwa viungo vya kitanzania kwa ajili ya watanzania, kuna mambo mengine mengi sana ya kikwetu kwetu kama muziki wetu wa bongo fleva, dansi zetu za kiduku, kandanda letu na ushindani wa Simba na Yanga, komedi yetu iliyo tofauti kabisa n.k. “
Kwa upande wake Diamond alisema kuwa “Kama ilivyo kauli mbiu ya tamasha hili ‘Kikwetu kwetu’ naamini nitatoa burudani kali kabisa kwa wanakigoma. Ukizingatia kuwa Kigoma ni nyumbani wanandugu zangu wategemee bonge la kiburudisho kutoka kwangu na wasanii wenzangu nitakaokuwa nao”.