Tamasha la ‘Kili Music Tour 2013’ ambalo linaandaliwa na Tanzania Breweries Limited (TBL) chini ya nembo yake ya Kilimanjaro Premium Lager, sasa linaelekea Mbeya ambapo wasaniii zaidi ya tisa watatikisa jiji hilo.
Tamasha hili kubwa litafanyika Jumamosi ya tarehe 24 Agosti, 2013 mjini Mbeya kwenye uwanja wa New City Pub na litajumuisha wasanii tisa ambao ni Linex, Fid Q ,Barnaba, Prof J, Kala Jeremiah, Ben Paul, Izzo Biz, Snura, na Awilo wa Mbeya
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa bia ya Kilimanjaro Bw George Kavishe alisema kuwa tamasha hilo linaelekea Mbeya baada ya kufanya vizuri jijini Mwanza na kuacha gumzo wiki nzima, kwa kufanyika tamasha la kukata na shoka.
“Tunashukuru kuwa watanzania wamepokea tamasha hili kwa moyo mkunjufu kabisa na walishiriki kikamilifu kwenye mikoa ya Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Mwanza,” Alisema Bw Kavishe.
Bw Kavishe alisema kuwa lengo kubwa ya tamasha hili ni kuondoa dhana kwa mtanzania kwamba kila kitu kinafanyika Dar es Salaam, basi tunategemea Mbeya itajumuika katika tamasha hilo ipasavyo.
Bwana Kavishe aliendelea kufafanua kuwa bia ya Kilimanjaro Premium Lager inaendelea kutoa bonge la kiburudisho kwa watanzania kwa kuhakikisha kuwa kila mkoa unapelekewa wasanii mahiri kabisa wa muziki wa bongo fleva.
Kwa niaba ya wasanii wenzake msanii mahiri wa muziki wa Hip Hop Fareed Kubanda maarufu kama Fid Q amewataka wakazi wa Mbeya kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya New City Pub.
“Tumejiandaa vizuri sana kutoa burudani kali kabisa, lazima mji wa Mbeya utikisike kwa kishindo cha bonge la kiburudisho kwa style tuipendayo ya “kikwetukwetu,” alisema Fid Q.
Ziara ya washindi na washiriki wa tuzo za muziki za ‘Kili Music Tour 2013’ zilianza mwanzoni mwa mwezi July na wasanii hao walizunguka katika mikoa ya Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Mwanza.