Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, leo alifkishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoani Morogoro kujibu mashitaka matatu yanayomkabili ambayo ni kutotii amri halali, kutoa maneno yenye nia ya kuharibu imani za dini na kushawishi kutenda kosa.
Shekhe Ponda amefikishwa mjini Morogoro na helkopta ya jeshi la polisi majira ya saa tano asubuhi chini ya ulinzi mkali ambapo askari waliimarisha ulinzi kwa muda wote huku kikosi cha kutuliza ghasia, FFU, wakiwa na silaha, mabomu na mbwa, ambapo hali hiyo imesababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli zingine za kiofisi katika ofisi zilizopo jirani na mahakama ya hakimu mkazi wakati kesi hiyo ikiendelea.
Akisoma shtaka mbele ya hakimu mkazi Richard Kabate, wakili mkuu wa serikali kanda ya Morogoro Benard Kongola amedai kuwa Sheikh Ponda anadaiwa kutenda makosa hayo matatu Agosti 10 mwaka huu majira ya jioni katika viwanja vya shule ya msingi kiwanja cha ndege manispaa ya Morogoro.
Katika shitaka la kwanza, sheikh Ponda anadaiwa kutotii amri halali ambapo shitaka la pili anadaiwa kutoa maneno yenye nia ya kuharibu imani za dini kwa kutoa maneno kuwa serikali iliamua kupeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wa Mtwara ni Waislamu.
Shitaka la tatu linalomkabili Sheikh Ponda ni kushawishi na kutenda kosa ambapo anadaiwa kuwa alitoa maneno ya ushawishi kwa kuwataka waislaam wasikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani zinaundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa CCM na serikali, na kama kamati hizo zitajitokeza aliwaamuru wafunge milango na madirisha ya misikiti kuwapiga.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo Sheikh Ponda anayetetewa na mawakili wasomi Barthoromew Tarimo na Ignas Punge alikataa mashtaka yote matatu na hivyo upande wa mashitaka kupinga dhamana kwa madai kuwa Sheikh Ponda anatumikia kifungo cha nje na kwamba hakutakiwa kufanya kosa, hata hivyo anakabiliwa na makosa mengine.
Upande wa mashitaka umedai kuwa upelelezi umekamilika na kesi hiyo itasomwa tena Agosti 28 mwaka huu ambapo mstakiwa amerudishwa rumande kwa helkopta jijini Dar es salaam.