Hivi karibuni bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipitisha muswada wa sheria ya fedha iliyosainiwa na rais Jakaya Kikwete na kuanza kutumika kama sheria kuanzia tarehe 01 August 2013. Sheria hii imetaja chanzo kimojawapo cha mapato kama tozo ya shilingi 1,000 kwa kila laini ya simu (sim card).
Kama mwitikio wa sheria hii, wananchi wengi kwenye mitandao ya kijamii waliipinga tozo hii na kwa kupitia jukwaa la Change Tanzania, kuanzia tarehe 15 Julai 2013, juhudi zilianza za kukusanya maoni ya wananchi kwa njia mbili: kwa njia ya mtandao – online petition – na kwa njia ya kukusanya sahihi za wananchi mitaani.
Hadi kufikia tarehe 13 August 2013, Change Tanzania kwa njia hizi mbili imekusanya zaidi ya sahihi elfu nne (4,000) kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Morogoro, Manyara, Mwanza, Shinyanga, Singida, Songea, Zanzibar na mikoa mingine. Juhudi bado zinaendelea za kukusanya sahihi zaidi.
Wito wa kusitisha tozo/kodi hii imeainisha kwa kina ni kwanini wananchi wanaipinga ikiwa ni pamoja na kuwa kodi hii ya laini ya simu inamkandamiza mtanzania wa hali ya kawaida na wa hali ya chini ambao ni 67% ya wananchi wanaoishi chini ya kipato cha dola 1.25 (shs 2,000) kwa siku. Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya wamiliki wa laini za simu milioni 22, milioni 8 wanatumia chini ya shilingi 1,000 kwa mwezi. Wito huu umeeleza kuwa kuwaongezea mzigo wananchi hawa kwa kiwango ambacho tayari wanashindwa kumudu ni kuwanyima kabisa fursa ya kutumia huduma hii muhimu.
Sababu nyingine iliyotajwa kwenye wito huu ni kuwa kodi hii haifuati misingi ya kulipa kwa kadri ya matumizi na ni kodi kandamizi inayotozwa kwa wamiliki wa laini za simu wote kwa kiasi kimoja bila kuzingatia kiwango cha matumizi.
Wito huu unasisitiza kuwa hii inamkandamiza mwananchi wa hali ya chini kwa kumlazimisha kulipa kiwango kikubwa cha kodi ikiwa ni tofauti na mapato yake. Mfano uliotolewa kwenye wito huu ni wa mtu anayetumia shilingi laki tano kwa mwezi kama muda wa maongezi na yule anayetumia shilingi elfu tano - na tukilinganisha uwiano wa malipo haya na matumizi yao – basi yule anayetumia shilingi laki tano analipa 0.2% ya matumizi yake, ila yule anayetumia shilingi elfu tano anatozwa 20% ya matumizi yake.
Aidha wito huu pia umeainisha sababu nyingine ya kiuchumi kwani tayari kodi nyingi zimeongezwa kwenye sekta hii ya mawasiliano. Wito huu umesisitiza kuwa kodi hii ni juu ya ongezeko la kodi mbalimbali katika huduma za simu za mkononi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ushuru kutoka 12% kwenda 14.5% na pia kodi hii kutozwa kwa huduma zote ingawa awali ilitozwa kwa huduma ya matumizi ya kuongea. Wito huu unainisha kuwa hivi sasa utumiaji wa internet, kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu za mkononi unatozwa kodi, hivyo ongezeko hili pekee limeshafanya huduma za simu za mkononi kupanda gharama kwa kiasi kikubwa, na ongezeko la tozo/kodi ya shs 1,000 litazidi kuwaumiza wananchi.
Wito huu pia umependekeza kuwa mapato ya ndani yanaweza kupatikana kupitia njia zingine mbadala ikiwa ni pamoja na serikali kupunguza matumizi yake mengineyo (safari, posho, semina, manunuzi ya magari na kudhibiti ufisadi) na imetaja utafiti uliofanywa na Interfaith Standing Committee on Economic Justice and the Integrity of Creation mwaka jana uligundua kuwa kwa wastani Tanzania hupoteza dollar za kimarekani billion moja (takriban shs trilioni 1.8) kila mwaka kutokana na ukwepaji kodi, uhamishaji haramu wa fedha na misamaha ya kodi.
Sahihi hizi za wananchi ni fursa kwa mbunge au wabunge wataokuwa tayari kuitika wito wa wananchi, wapiga kura wao na kupeleka hoja bungeni kwa ajili ya kufuta tozo/kodi hii, tafadhali wawasiliane na CHANGE TANZANIA kwa namba zetu hapo chini. Pia unaweza endelea kuweka sahihi yako kupitia mtandao huu hapa.