PAZIA la shindano la kuimba la Epiq Bongo Star Search mwaka 2013, limefunguliwa rasmi mkoani Dodoma mwishoni mwa wiki hii, ambapo wakali sita wa fani hiyo wamepatikana katika usaili wa siku mbili uliofanyika katika ukumbi wa Maisha na kwa sasa linahamia Zanzibar kuanzia Julai 5 na 6.
Shindano hilo ambalo sasa liko msimu wa saba toka kuzinduliwa kwake, mwaka huu lina kauli mbiu mpya ya ‘KAMUA’, ambayo inahimiza vijana kujitokeza katika kuwania fursa zinazopatikana katika tasnia ya burudani.
Akizungumzia usaili wa mwaka huu jaji mkuu wa shindano hilo, Ritha Paulsen alisema kuwa mwaka huu shindano hilo limedhamiria kuwafikia vijana wengi zaidi ili kuwasaidia kufikia malengo yao kimuziki.
‘Leo tumepata wakali wetu ambao ni moja kati ya zile harakati zetu za kuwawezesha vijana ya kutimiza ndoto zao kama vijana wengine kadhaa waliofanikiwa, ambayo hakika ni changamoto kwa vijana waliojitokeza hapa kupambana kufika huko’ alisema Ritha.
Kwa upande wake Afsa Biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan, alisema idadi ya vijana iliyojitokeza Dodoma inaashiria umuhimu wa shindano hilo kwa jamii ya Tanzania.
‘Vijana waliojitokeza hapa wanaonyesha kuwa shindano hili linasaidia maisha yao, hali inayotusukuma tuzidi kuliboresha zaidi ili liwasaidie vijana wengi zaidi’ alisema Khan.
Mwaka jana mkoa wa Dodoma uliingiza mshiriki mmoja kwenye tano bora, ambaye ni Godfrey Levis, huku mwaka huu vijana wengi waliouhudhuria wakionyesha upinzani mkali.