Rais wa Marekani Barack Obama ambaye yuko katika ziara yake ya Afrika, amesifu nchi ya Senegal kwa kuwa moja ya nchi zenye demokrasia thabiti barani Afrika.
Akiwahutubia waandishi wa habari nchini Senegal kwa mkondo wake wa kwanza wa ziara yake Afrika,baada ya mazungumzo na rais Macky Sall, Bwana Obama alisema kuwa Senegal iliandaa uchaguzi huru na wa haki pamoja na kuwa na kipindi salama cha mpito.
Pia aliisifu kwa kuwa na mtindo wa kusuluhisha migogoro kwa mazungumzo na mashauriano, wala sio kwa njia ya ghasia.
Alisema kuwa Afrika kama bara limepiga hatua kubwa upande wa demokrasia katika miaka ya hivi karibuni.
Obama atazuru Afrika Kusini ambako rais mstaafu Nelson Mandela anaugua sana na amelazwa hospitalini. Aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanamuombea Mandela pamoja na familia yake.