BENDI ya Muziki wa dansi hapa nchini Mashujaa, inatarajia kuwatambulisha wapya sita katika hafla itakayofanyika kesho katika Ukumbi wa Zhonghua Garden Morocco Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja wa bendi hiyo Martine Sospter alisema, wapya hao kutoka Kongo wanne ni wanenguaji na wawili ni waimbaji ambao watasaidiana kazi ili kuimalisha bensi hiyo.
Sospter alisema, mbali na utambulisho huo, watatumia siku hiyo kuwashukuru Watanzania kwa kuwateua hadi kuibuka bendi bora ya mwaka katika kinyang’anyiro cha Kill Music Award kilichofanyika hivi karibuni.
“Sisi tunamshukuru mungu kwa kutufanya kuwepo imara mpaka sasa, na hatutawaangusha mashabiki wetu kwani tunaukubali sana mchango wao wa hali na mali na ndio maana tunawaomba wajitokeze kwa wingi Jumamosi ili wajionee mambo mapya ikiwemo kuwatambulisha wasanii wapya na wanenguaji,”alisema Sospter.
Aliongeza kuwa siku hiyo Msanii wa kizazi kipya Dully Sykes atawasindikiza katika hafla hiyo.
Nae Mratibu wa bendi hiyo, Kingdodoo Bouche aliwataja wapya hao kuwa ni, Gracia Mesu a.k.a John Boko, Bosawa Fany ‘Juma Kaseja’, Jolie Kindu ‘Mrisho Ngasa’ na Patricia Nzomba ‘Mbwana Samata’ huku waimbaji akiwa ni Jimmy Adoli na Eddy Mboyo.
Aliongeza kuwa kwa kuwa bendi yao ni imara na ni ya utaifa ndo sababu ya wanenguaji hao kutumia majina ya wachezaji wa timu ya Taifa
‘Taifa Stars’.