Quantcast
Channel: HABARI NA MATUKIO
Viewing all articles
Browse latest Browse all 19575

JINSI YA KUJIKINGA NA UGONJWA WA KISUKARI

$
0
0
Kisukari ni hali inayotokea wakati sukari inapozidi ile inayotakiwa katika damu kwa sababu ya upungufu au ukosefu wa insulin. Insulin ni kichocheo kinachotengenezwa kwenye kongosho na kwamba hutumika kusaidia mwili kutumia sukari inayotokana na vyakula tunavyokula.

Aina za kisukari Kuna aina kuu mbili za kisukari;

Kwanza ni kisukari kinachotegemea insulin. Insulini ni aina ya homoni inayozalishwa na kongosho. Kazi a Insulini ni kurekebisha hali ya sukari kwenye damu, ikiwa ni nyingi inapunguzwa kurudi kwenye hali ya kawaida na ikiwa chache huruhusu irejee kwenye hali ya kawaida pia.Kunapokuwa na hitilafu kongosho likazalisha homoni hii kwa wingi, sukari hupungua mwilini, au isipozalishwa, sukari huongezeka mwilini.Hospitalini, aina hii ya sukari inatibiwa kwa kutumia sindano za insulin na kurekebisha ulaji wa vyakula.

Pili ni kisukari kisichotegemea insulini. Hospitalini hiki hutibiwa kwa kutumia vidonge pamoja na kurekebisha ulaji wa vyakula au kwa kurekebisha vyakula peke yake. Watu wengi walio na aina ya kisukari kisichotegemea insulin ni wanene kupita kiasi na ikiwa watapunguza uzito kasi ya ugonjwa hupungua au kuisha kabisa.Sukari inaweza kuwa juu au chini kupita kiasi cha kiwango kinachotakiwa.

Hali zote hizo mbili si nzuri kwa binadamu kwa sababu mgonjwa anaweza kufa haraka.Sukari inaweza kuwa juu bila dalili zozote zile kujitokeza mwilini mwa mgonjwa. Watu wanaojijua kuwa na tatizo la kisukari wanashauriwa kupima damu au mkojo mara kwa mara ili kufahamu kama sukari katika damu yao iko sawa au haiko sawa.

Dalili za mtu aliyepungukiwa sukari mwilini ni pamoja na mapigo ya moyo kwenda haraka haraka, kutokwa jasho kwa wingi, kujisikia kama mwenye homa, kuchoka na kuumwa kichwa. Ni vizuri mtu akihisi dalili hizo ahakikishe anapima sukari mwilini. Hadi sasa hakuna tiba ya kuponya ugonjwa wa kisukari.

Hata hivyo wagonjwa wote wanaweza kuishi vizuri na kufanya kazi zao zote ikiwa watafuata maelekezo na masharti yanayotakiwa. Madhara ya kisukari Mtu mwenye kisukari anaweza kupatwa na tatizo la kupungua uwezo wa macho kuona, figo kutofanya kazi zake ipasavyo na kupata vidonda vya miguuni visivyopona.

Pia mtu mwenye tatizo la kisukari mishipa yake ya fahamu ya miguuni na mikononi kutofanya kazi zake vizuri, matatizo ya moyo na kupatwa na magonjwa mbali mbali ya ngozi. Madhara hayo yanazuilika kwa kuzingatia kutozidi kwa sukari kwenye damu ya mgonjwa.

Ushauri kuhusu chakula kama una kisukari na hujatibiwa Vyakula vinavyofaa husaidia mwili kuwa na viwango vya sukari na mafuta vinavyostahili kuwepo damuni, hupunguza unene kupita kiasi, hutosheleza mahitaji ya mwili ya nishati, madini na vitamini ili kuuwezesha mwili kuwa na uzito unaostahili na kufanya kazi ipasavyo.

Kila mwenye tatizo la ugonjwa wa kisukari anatakiwa kuepuka kula vyakula vilivyowekwa sukari kwa sababu sukari huyeyushwa upesi sana tumboni na kusababisha sukari nyingi kuingia kwenye damu katika muda mfupi. Vyakula kama sukari, glucose, asali, jamu, keki, pipi, ice cream, chocolate na soda zote zilizo tamu haviruhusiwi kwa mtu mweye tatizo la kisukari. Chai, kahawa, maziwa na uji vinaruhusiwa kutumiwa iwapo vitakuwa havijaongezwa sukari. Madafu na club soda vinaruhusiwa kwa sababu havina sukari inayoweza kuyeyuka haraka na kukimbilia kwenye damu.

Mgonjwa wa sukari anaweza kuongeza utamu kwenye mchanganyiko anaoutaka kwa kutumia vidonge ambavyo hupatikana kwenye maduka ya madawa.Njaa nayo huchangia kumfanya mgonjwa wa kisukari kujisikia vibaya huenda kwa vile sukari inaweza kupungua kupita kiasi mwilini.Mgonjwa wa kisukari anatakiwa kutokaa na njaa, kula mara kwa mara na pia kula mara tatu au zaidi kwa siku na ikiwezekana anatakiwa kutafuna vitu vidogo vidogo katikati ya milo mikubwa.

Inashauriwa kuwa mgonjwa asipendelee kula milo mikubwa mchana au jioni. Mgonjwa huyo hatakiwa kuacha kula vyakula vyenye wanga kama vile ugali, viazi na wali. Anachotakiwa kufanya ni kuzingatia kiasi cha chakula cha wanga anachokula kwa mlo na pia anatakiwa kutumia zaidi nafaka zisizokobolewa kwa mfano dona kwa sababu huweza kumpatia mgonjwa vitamini na madini. Hakuna sababu ya mgonjwa kupikiwa chakula chake maalum kwa sababu anaweza kula chakula chochote kilichopikwa na familia isipokuwa vile vilivyowekwa sukari.

Mgonjwa anatakiwa kula matunda kwa wingi na kwamba anaweza kula matunda aina zote kwa siku. Anatakiwa pia kula mboga za majani kwa wingi au kachumbari kila siku. Mgonjwa wa kisukari anatakiwa kupunguza kiasi cha mafuta anachokula na pia kuepuka kula mafuta yenye asili ya nyama. Anatakiwa kutumia zaidi vyakula vilivyochomwa, kuokwa au kubanikwa kuliko vile vilivyokaangwa na kula samaki, maharage au kuku aliyetolewa ngozi.

Mgonjwa wa kisukari anatakiwa kuepuka kunywa pombe kwa wingi kwa sababu huweza kuathiri afya yake.Kama mgonjwa huyo hawezi kujizuia iwapo ni mnywaji wa bia, anatakiwa kunywa chupa moja au mbili na sio zaidi ya hizo, kama ni mvinyo anatakiwa kunywa bilauri moja au mbili tu au toti nne za vinywaji vikali kwa siku.

Vyakula vya hatari kwa mgonjwa Vyakula vinavyoweza kumwongezea mgonjwa madhara ni sukari yenyewe, nyama nono yenye mafuta, mayai, figo au maini husababisha sukari kupanda kwa kiwango cha aina ya mafuta mabaya yanayosababisha damu kuganda kwenye moyo na mishipa ya damu na kuleta magonjwa ya moyo. 

Vyakula vya kuliwa bila mashariti Mboga za majani, nyanya, matango, bamia, karoti, vitunguu, pilipili hoho, pilipili, viungo vyote vya vyakula bila kuweka chumvi nyingi, maji ya kunywa, chai na kahawa.Ikiwa mgonjwa wa kisukari anaumwa na hawezi kula vyakula vya kawaida anatakiwa kunywa uji, maziwa, chai, kahawa, na kuongeza sukari. Maji ya matunda au vyakula baridi na kula miwa kama inapatikana. Kila mgonjwa wa kisukari anashauriwa kwenda kupata ushauri wa madaktari na pia kufanya mazoezi.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 19575

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>