Askari Magereza Ramadhan Mussa (54) enzi za uhai wake.
Na Hillary Shoo, SINGIDA.
WATU wanne wamefariki dunia Mkoani Singida katika matukio tofauti likiwemo la askari magereza mmoja wa Mkoa wa Singida kufa baada ya kupata ajali mbaya ya gari lake dogo kugongana uso kwa uso na lori usiku.
Kamanda wa polisi Mkoani hapa Geofrey Kamwela alisema askari magereza wa huyo ametambuliwa kuwa ni Staff Sagenti Ramadhan Mussa (54) alikufa papo hapo baada ya gari lake alilokuwa akiendesha kuacha njia na kugongana na lori barabara kuu ya Singida Dodoma.
Alisema marehemu alikuwa akitokea maeneo ya Misuna majira ya saa 3: 00 usiku akitumia gari lake dogo aina ya Toyota Mark II lenye namba za usajili T 734 AEX .
Alisema akiwa njiani inadaiwa alikuwa akimkwepa mwendesha kibajaji na ndipo aligongana uso kwa uso na lori lenye namba za usajili T 256 CVN aina ya MAN likiwa na tela lenye namba za usajili T 175 CWS lililokuwa likitokea Kahama kwenda Dar es Salaam.
Gari likiwa limeharibika kwa mbele na kusababisha kifo cha askari magereza huyo papo hapo.
Katika tukio la pili watu wawili wakazi wa kijiji cha Rungwa Tarafa ya Itigi Wilayani Manyoni wameuawa na wananchi wenye hasira kali wakituhumiwa kwa wizi.
Kamanda Kamwela aliwataja marehemu kuwa ni Chritofa Kamungenge (37) na Mussa Daniel (32) wote wakazi wa kijiji cha Rungwa ambao waliopata majeraha mbalimbali katika miili yao na walifariki wakati wakipatiwa matibabua hospitali ya wilaya ya manyoni.
Alisema chanzo cha mauaji hayo ni kuwa siku ya tukio Septemba 06 mwaka huu kuna maduka mawili yalivunjwa na kuibuwa vitu mbalimbali na baada ya msako marehemu walikutwa na baadhi ya mali zilizoibiwa kwenye duka moja kijiji hapo.
Katika tukio la tatu huko katika kijiji cha Ntondo Kata ya Msisi Singida vijijini mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Ntondo Yasin Shaban (10) alifariki dunia baada ya kukandamizwa na tawi la mti alilokuwa akikata.
Chanzo cha kifo hicho ni uzembe wa mwanafunzi huyo kukata tawi la mti bila tahadhari ambapo tawi lilifyatuka gafla na kumbamiza kichwani upande wa shavu la kushoto na kupelekea kifo chake.
Gari linavyoonekana kwa mbele.
Askari magereza wakilinda gari hilo eneo la kibaoni.
Magari yakiendelea na safari zake baada ya lori lililogongwa na gari hilo dogo kuondolewa eneo la ajali jana.
Diwani wa viti maalumu Kata ya Kindai Mwajuma Shaha (aliyeshika mkoba)akiangalia gari dogo la askari magereza likiwa nje ya barabara baada ya kugonga lori kwa mbele uso kwa uso. (PICHA ZOTE NA HILLARY SHOO WA MOblog SINGIDA).